FARIDA MANGUBE, MOROGORO
FURAHA, matumaini na heshima vilitawala katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) leo Mei 22, 2025 jumla ya wahitimu 794 walitunukiwa shahada mbalimbali katika mahafali ya 45 ya chuo hicho.
Wahitimu hao walipokea Shahada za Awali, Shahada za Umahiri, Shahada za Uzamili na Shahada za Uzamivu (PhD), wakitoka katika fani mbalimbali zinazolenga kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo, mazingira na maendeleo ya jamii. Kati yao, wanaume walikuwa 495 na wanawake 299, sawa na asilimia 37.7.
Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Doroth Mwanyika kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza, Andrew Massawe, aliwataka wahitimu kutumia maarifa waliyoyapata kuchochea mabadiliko chanya katika jamii zao.
“Katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi, elimu mnayobeba ni nyenzo muhimu ya kuona fursa mpya, kujiajiri na kuwasaidia wengine kupata ajira,” alisema Mwanyika.
Aliongeza kuwa Baraza la Chuo katika kikao chake cha awali liliridhia kuongeza msisitizo katika mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanahitimu wakiwa tayari kushindana katika soko la ajira na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Makamu wa Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda, aliwataka wahitimu kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kutumia elimu yao kwa manufaa ya watu wengi, huku akisisitiza kuwa kuhitimu SUA ni matokeo ya juhudi na nidhamu ya hali ya juu.
“Kumaliza masomo SUA si jambo rahisi. Ni matokeo ya kujituma kwa wahitimu na pia msaada mkubwa kutoka kwa wazazi na walezi wao,” alisema Prof. Chibunda huku akiwapongeza wote waliokamilisha safari hiyo ya kielimu.
Mahafali hayo yalihitimishwa kwa zoezi la kutunuku rasmi lililoongozwa na Mkuu wa Chuo hicho, Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba, aliyepongeza juhudi za wahitimu na kuwataka kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii..jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment