Na Mwandishi wetu, Mbulu
VIKUNDI 49 vya wanawake wajasiriamali waliopo kwenye Halmashauri ya Mji wa Mbulu Mkoani Manyara, wanatarajia kupatiwa mikopo ya Sh168 milioni.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Rehema Bwasi ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha robo tatu ya mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Bwasi amesema vikundi hivyo vimeshafanyiwa ukaguzi na uhakiki na kudhibitishwa na maofisa wa benki watakayochukulia mikopo yao.
Amesema awali waliandikisha vikundi 66 kwa ajili ya kupatiwa mikopo ya Sh233 milioni ila baada ya maofisa wa mikopo wa benki kuwachuja vikabakia vikundi 43 vitakavyopata Sh168 milioni.
Amesema wamejipanga kuhakikisha vikundi vya wajasiriamali ambavyo havijakidhi vigezo vinarekebisha mapungufu ili na vyenyewe viweze kunufaika na mikopo hiyo.
Amesema maofisa wa mikopo wa benki walitembelea vikundi vyote 66 vya wanawake wajasiriamali na kukagua kikundi kimoja hadi kingine na kubaini vikundi 17 havijakidhi vigezo.
"Kuna utaratibu ulipaswa kufanyika ambao haukukamilika na maofisa mikopo wa benki wamebainisha na utarekebishwa ili wajasiriamali hao wanufaike," amesema Bwasi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbulu, Peter Sulle amesema changamoto walizokutana nazo wanakikundi wengine ambao hawapo kwenye mpango wa kupatiwa mikopo zifanyiwe kazi ili nao wanufaike.
"Hao wajasiriamali wengine ambao hawajafanikiwa kupitishwa katika orodha ya watakaopatiwa mikopo wasaidiwe kurekebisha mapungufu ili nao waweze kunufaika ili kujiinua kiuchumi," amesema Sulle.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Alexander Tango amesema anatarajia wajasiriamali watanufaika kwani wao wapo katika mpango wa kitaifa katika utoaji mikopo kupitia benki.
"Halmashauri ya mji wa Mbulu tupo kwenye mpango wa kitaifa tunatarajia wajasiriamali wetu hawatatuangusha katika kurejesha mikopo hiyo," amesema Tango.
Mkazi wa mji wa Mbulu, Veronica Michael ameipongeza hatua hiyo kwani itachochea katika kunyanyua uchumi wa wanawake hao ambao ni nguzo za familia.
Amesema kupitia mikopo hiyo uchumi wa wanawake hao na jamii kwa ujumla utaonekana kupitia ujasiriamali utakaofanywa na vikundi hivyo.
No comments:
Post a Comment