HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 26, 2025

Ulinzi wa Miundombinu ya Mawasiliano Wapewa Kipaumbele katika Maendeleo ya Kidigitali

 







*UCSAF yaonya dhidi ya uharibifu wa minara ya mawasiliano, yaahidi kuimarisha uhamasishaji wa jamii

SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeweka msisitizo mkubwa katika ulinzi na utunzaji wa miundombinu ya mawasiliano, ikibainisha kuwa uharibifu wa minara una athari kubwa kwa maendeleo ya taifa na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema minara 533 kati ya 758 iliyopangwa kujengwa tayari imewashwa, sawa na asilimia 70.32 ya utekelezaji kufikia tarehe 23 Mei 2025. Hata hivyo, ameonya kuwa mafanikio haya yanaweza kudhoofika iwapo wananchi hawatashirikiana kulinda miundombinu hiyo muhimu.

“Miundombinu ya mawasiliano ni mali ya umma. Tunatoa wito kwa wananchi kuilinda kwa kuwa uharibifu wake unasababisha hasara kubwa kwa taifa na kuchelewesha maendeleo,” amesema Mwasalyanda.

Ameongeza kuwa UCSAF itaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa miundombinu hiyo na nafasi yake katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan kwa vijana na wakazi wa vijijini.

Katika juhudi za kufikia Watanzania wengi zaidi, UCSAF imeshatekeleza miradi katika kata 1,661 zenye vijiji 4,570, kwa kujenga minara 1,810 inayotoa huduma za simu, intaneti na huduma nyingine za kidigitali kwa takribani watu milioni 25.1.
Serikali imetenga shilingi bilioni 126 kwa ajili ya kukamilisha jumla ya minara 758, ambayo inatarajiwa kuhudumia wananchi milioni 8.5 katika kata 713, wilaya 127 na mikoa 26 nchini.

Kwa mujibu wa Mwasalyanda, serikali inaendelea kushirikiana na watoa huduma kuhakikisha huduma hizo zinafika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, huku vijana wakihimizwa kutumia fursa hizi za kidigitali kwa maendeleo yao na ya jamii zao.

“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika safari ya kuelekea uchumi wa kidigitali. Lakini hilo linawezekana tu kama jamii itakuwa mshirika wa kweli katika kulinda na kuthamini miundombinu hii,” amesema Mhandisi Mwasalyanda.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad