Na Janeth Raphael - MichuziTv Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolph Mkenda amesema kuwa mabadiliko na maboresho yaliyofanywa katika mitaala ya elimu ya awali,msingi na Sekondari ni pamoja kuanzishwa kwa somo la lazima la biashara na Historia ya Tanzania pamoja na kuweka mikondo miwili ya Elimu ya sekondari yaani mkondo wa jumla na mkondo wa Amali.
Prof. Mkenda ameeleza hayo leo Jijini Dodoma Mei 27,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akielezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Na kuongeza kuwa, kwa upande wa elimu ya ufundi mitaala 389 na mitaala 563 ya elimu ya juu imeanzishwa na kuboreshwa ili kuendana na Sera hiyo.
"Sambamba na Sera Tumefanya mabadiliko na maboresho katika mitaala ya elimu Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu. Mabadiliko makubwa ni pamoja na kuweka mikondo miwili ya Elimu ya Sekondari Mkondo wa Jumla na Mkondo wa Amali na kuweka mfumo wa elimu kuwa nyumbufu. Aidha".
"katika mitaala hii tumeanzisha somo la lazima la elimu ya Biashara na Historia ya Tanzania pamoja na kuimarisha mifumo ya ufundishaji lugha. Hali kadhalika upande wa elimu ya ufundi mitaala 389 na elimu ya juu Mitaala 563 imenzishwa na kuboreshwa ili iendane na Sera na kuzingatia stadi za karne ya ishirini na mahitaji ya kiujuzi kitaifa kikanda na kimataifa. Msemo mkubwa sasa katika jamii ni Elimu na ujuzi ndio mpango mzima".
Aidha amesema Serikali imeongeza fedha za Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya Juu kutoka 570 bilioni - 2021/22 hadi 787 bilioni 2024/25 huku Jumla ya wanufaika ikiongezeka kutoka wanafunzi 177,925 mwaka 2021/22 hadi wanafunzi 248,331 mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 39.6 sambamba na uondoaji wa TOZO ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha katika urejeshaji mikopo na Tozo ya adhabu ya asilimia 10 iliyokuwa inatozwa waliochelewa kulipa mkopo na pia ongezeko la fedha za kujikimu kutoka sh. 8,500 hadi shilingi 10,000 kwa siku.
Tarehe 1 Februari 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023.
No comments:
Post a Comment