HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 26, 2025

PPP, REDET WAANDA KONGAMANO KUJADILI UBIA KATI YA SEKTA YA UMMA, BINAFSI KUELEKEA DIRA YA UCHUMI MWAKA 2050

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

KITUO cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi(PPP) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET)chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) wanatarajia kufanya kongamano litakaloshorikisha wasomi wa kada mbalimbali kwa ajili ya kupata mtazamo wa pamoja kuhusu ubia kati ya sekta ya umma na binafsi kuelekea dira ya 2050.

Katika kongamano hilo litakalofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutakuwa na mada ndogo tatu ,mada ya kwanza ni mada itatolewa na Mkurugenzi Mkuu wa PPP David Kafulila ambaye ataelezea dhana ya PPP na nafasi yake katika kuelekea dira ya 2050.

Akishamaliza kuwasilisha kutakuwa na mjadili mada ambaye atakuwa Profesa Anna Tibaijuka,mada ya pili itakuwa ni Sekta binafsi na Mitaji kutoka nje katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania hii itakayowasilishwa na Profesa Abel Kiondo ambaye ni Profesa wa Uchumi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam katika idara ya uchumi.

Baada ya hapo hii mada yake itajadiliwa na Dk.Jamal Msami yeye ni Mkurugenzi katika Taasisi ya REPOA na mada ya tatu itakuwa nafasi ya PPP katika kukuza uwekezaji na ufanisi katika Serikali za mitaa kama wote tunavyojua Serikali za mitaa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kuhusu kongamano hilo,Mkurugenzi Mkuu wa PPP David Kafulila ametumia nafasi hiyo kualika wasomi wa kada mbalimbali kushiriki kongamano hilo ambalo linalenga kubadilishana mawazo na hatimaye kuwa na fikra ya pamoja kuhusu mtazamo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

“Tunaufahamisha umma kupitia vyombo vya habari kwamba tutakuwa na mdahalo au kongamano kwa ajili ya kujadili nafasi ya sekta binafsi na sekta ya umma kuelekea uchumi wa mwaka 2050 ambao siku chache zijazo mpango wake au dira yake utakwenda kuzinduliwa

“Kwa hiyo sisi kama Kituo cha ubia tunaowajibu wa kile kinachoitwa ushirikishaji wa Umma kwenye masuala ubia na ubia nadhani mnafahamu ni mikataba ya muda mrefu ya kutumia sekta binafsi ambayo kimsingi ilikuwa ni Serikali iyafanye…

“Ni jukumu la Serikali kujenga barabara ,ni jukumu la Serikali kuzalisha umeme,ni jukumu la Serikali kuendesha bandari lakini kwasababu tofauti ambazo zitajaliwa kwenye kongamano hilo Serikali huwa inaipa sekta binafsi kutekeleza kwa utaratibu huu unaoitwa uratibu wa ubia

“Kwahiyo Kituo cha ubia kinawajibu wa kushirikisha umma kuhusu masuala haya kwa lengo la kujenga uelewa unaofanana kati ya Serikali na wananchi ili kuwa na mtazamo unaofanana.Serikali inatekeleza haya kwa niaba ya wananchi kwa ajili ya umma.

“PPP moja ya wajibu wetu ni kujenga ushiriki wa kufanya umma uelewe masuala ya kisera, kisheria na mipango ya serikali kwenye maeneo hayo ya ubia .Hivyo tumeona ipo haja ya kushirikiana na taasisi kubwa na muhimu kama REDET ambayo imebobea katika uendeshaji wa haya makongamano .

“Kwa kwa kushirikisha lakini zaidi kufanya wanazuoni wa Tanzania waelekeze fikra katika eneo hili kwa lengo la kuhakikisha tunafikiria katika namna inayofanana kati ya Serikali, na wanazuoni tunapozungumza masula ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.”

Kafulila ameongeza kuwa mdahalo wa kesho Mei 27 mwaka huu msingi wake ni huo na wao wanatimiza wajibu wao kama Kituo cha ubia kufanya ushirikishaji kwa umma katika masuala ya kisera ,kisheria pamoja na programu za masuala ya ubia kwa lengo la kuhakikisha wanapata mawazo, changamoto na mitazamo kuhusu namna kufanya vizuri zaidi.

Amefafanua wanafahamu Serikali inakwenda kuzindua hiyo Dira ambayo inalenga kujenga uchumi utakaofika Dola takribani trilioni moja katika miaka 25 ijayo.Uchumi ambao wanauzungumzia ukubwa wake ni sawa sawa na nchi 19 tu duniani ambazo kwa sasa zimefikia kiwango hicho.

“REDET wanaofanya vizuri katika kuendesha kongamano na wamefanya vizuri kwa miongo mingi sasa, kwahiyo sisi tukaona kwamba tuweze kufanya kazi kwa pamoja kupitia Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kwa lengo la kuhakikisha wanazuoni wanatoa mchango wa kutosha katika mtazamo wa Serikali kuelekea dira ya uchumi 2050.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa REDET Profesa Rwekaza Mukandala amesema kama wanavyojua ubia kati ya dola, Serikali na sekta binafsi na kama au panga lenye makali sehemu zote mbili , hivyo zinakata sehemu zote.

“Kwahiyo ukishika vizuri huo upanga kwa kuelewa unakata wapi utapata manufaa lakini kama huna uelewa wa kutosha unaweza ukajikata na ukawa na madhara,Hivyo sisi pamoja na Kituo cha ubia tunataka kuongeza ufahamu,uelewa wa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma na dola…

“Kwa kufikiria kwa pamoja wanazuoni ,watendaji wa Serikali , washiriki kutoka vyama vya siasa, vyombo vya habari ,taasisi zisizokuwa za Serikali ambapo kwa pamoja tutachambua,kudadavua na kukuza uelewa wetu wa upanga huu ambao ni muhimu.

“Matarajio yetu ni kuwa na maendeleo ya kasi zaidi na hivyo lazima kushirikisha sekta binafsi lakini kwa uangalifu mkubwa bila kuogopa ,tuwe jasiri lakini ujasiri ambao unajengwa na msingi wake ni mzuri,shirikishi.” Amesema huku Akieleza kuhusu mada ambazo zitajadiliwa katika kongamano hilo ambalo amesisitiza ni la wazi na wengi wanatarajiwa kushiriki.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad