NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) upande wa miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila amelipongeza Shirika la Amend pamoja na washirika wake kwa juhudi zao za kuhakikisha usalama barabarani kwa wanafunzi nchini Tanzania na barani Afrika na kusaidia kulinda maisha ya viongozi wa kizazi kijacho.
Akizungumza leo Mei 29, mwaka huu wakati wa hafla ya uzinduzi wa uboreshaji miundombinu salama kwa watoto shuleni iliyojengwa katika Shule ya Msingi Sinza maalum jiiini Dar es Salaam Mhandisi Mativila aliyemwakilisha Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa, amesema ni muhimu kuunga mkono mipango inayolenga kuwalinda watoto hasa wenye ulemavu na mahitaji maalum.
“Nina matumaini mipango tunayoadhimisha leo itachangia mazingira salama kwa watoto wa shule hii ya Sinza Maalum na jamii kwa upana zaidi. Kwa kupunguza kasi ya vyombo vya moto, kujenga njia za watembea kwa miguu, vivuko vya pundamilia na alama mbalimbali, tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya ajali za barabarani na kuokoa maisha.
“Katika jukumu langu, nimejitolea kukuza wazo kwamba watoto ndio rasilimali yetu ya thamani zaidi. Inasikitisha kusikia watoto wakijeruhiwa au kuuawa katika ajali za barabarani. Lazima tufanye kila tuwezalo kuzuia majanga kama haya. Tukio hili hii leo linatoa fursa nzuri ya kuangazia umuhimu wa kuzuia ajali za barabarani kupitia miundombinu salama,”amesema.
Ameongeza watoto wote wanastahili safari salama ya kwenda shule ili waweze kuendelea kujifunza na kukua na kufaulu katika siku zijazo. Kwa bahati mbaya, mara nyingi kwenda na kurudi shuleni zitakuwa safari hatari kwa watoto kama hatutaendelea kuchukua jitihada kama hizi, haswa katika maeneo ambayo hayana miundombinu salama kwa watembea kwa miguu.
Aidha, amesema madereva lazima watii sheria zote za barabarani - kuendesha gari kwa mwendo unaoruhusiwa kisheria, hasa katika maeneo yenye wakazi wengi, na kuepuka kutumia vilevi wawapo barabarani huku akisisitiza ufuataji wa sheria ni muhimu pia.
“Sote tuna jukumu la kutekeleza katika kuhakikisha watoto wetu wote wanafika na kutoka shuleni kwa usalama kila siku. Wizara yangu inaunga mkono jitihada hizi na tutaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha tunajenga barabara salama kwa watumiaji wote wa barabara…
“Hasa wanafunzi katika maeneo ya shule kama na kuweka mazingira rafiki kwa wadau kama Amend na FIA Foundation kuunga mkono jitihada hizi ilikuokoa maisha katika barabara zetu, hasa maisha ya watoto wetu. Natumai kuwa ushirikiano imara uliojengwa wakati wa mradi huu katika Shule ya Msingi ya Sinza Maalum utakuwa msingi wa ushirikiano wa siku zijazo kati ya wadau katika ngazi zote.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo amesema katika uzinduzi huo nchi tisa zimeshuhudia tukio na kutumia nafasi hiyo kueleza mradi huo wa uboreshaji wa usalama barabarani katika shule ya msingi yenye watoto wenye mahitaji maalumu ni wa kwanza kuushuhudia katika kipindi cha miaka 13 ambayo wamekuwa wakitekeleza miradi hiyo.
“Kwa kweli ninafahamu jukumu kubwa linalowakabili wazazi, walezi na walimu wa watoto hawa, hivyo naamini maboresho yaliyofanyika hapa sio tu yatapunguza hatari ya ajali za barabarani bali pia yatawatiamoyo wazazi kuwaleta watoto hawa shuleni, angalau wapatefursa ya kujifunza.
“Duniani kote, ajali za barabarani husababisha karibu vifo milioni 1.3 vinavyoweza kuzuilika na wastani wa majeruhi milioni 50 kila mwaka, na hivyo kufanya ajali za barabarani kuwa chanzo kikuu cha vifo vya watoto na vijana (5-29 yrs) ulimwenguni kote.
“Afrika ina viwango vya juu zaidi vya vifo vya barabarani kuliko bara lolote ingawa tuna idadi ndogo zaidi ya magari kulinganisha na mabara mengine. Watoto hasa wanafunzi wako katika hatari zaidi, kwani wengi hutembea kila siku kwenda na kurudi shuleni.
“Takwimu hizi hazikubaliki, na hatua za haraka zinahitajika. Hakuna mzazi anayependa kushuhudia mtoto wake akipoteza maisha au kujeruhiwa wakati akienda shuleni moja ya safari muhimu sana kwa watoto hawa, kwani shuleni ndiko kunako wafunguliwa maisha yao ya baadaye,”amesema Kalolo.
Pia amesema katika Shule ya Msingi Sinza Maalum kupitia mradi wa uboreshaji moundombinu salama kwa watoto ,wameweka vivuko vya pundamilia, matuta ili kupunguza spidi, alama za barabarani pamoja na njia za watembea kwa miguu.Kwa aina ya mradi huu shule 100 barani afrika na 59 nchini Tanzania ikiwa ni zaidi ya wanafunzi 52,793, na 102,821 barani Afrika.
Wakati huo huo Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge amesema tatizo la ajali limekuwa kubwa Kinondoni na kutolea mfano Hospitali ya Mwanyamala kuwa imekuwa ikipokea watu wawili waliopoteza maisha kila siku kutokana na ajali hali ambayo ni sawa na vifo 60 kwa mwezi.
“Wengi ni vijana na watoto. Madereva wengi hawafuati alama za barabarani, na baadhi ya waendesha bodaboda hawasimami kwenye vivuko. Tunahitaji hatua zaidi,” amesema.
Awali Mwakilishi wa Jeshi la Polisi kutoka Kitengo cha Usalama Barabarani, SSP Mbunja Matibu amesema jeshi hilo linaendelea kutoa elimu ya usalama kwa watoto na watu wazima, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na jamii.
“Tunatoa elimu mashuleni kwa watoto namna ya kuvuka barabara kwa usalama. Lakini pia tunahimiza watu wazima kuwavusha watoto, na abiria kuwajibika kwa kuwasimamia madereva wanaovunja sheria.”
Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam anayeshughulikia Elimu Abedi Milanzi alisema maboresho hayo yamepunguza adha kubwa kwa watoto wenye mahitaji maalum.



No comments:
Post a Comment