HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 24, 2025

MBEKI AWAASA VIONGOZI WA AFRIKA KUWA WAZALENDO KATIKA KULINDA MASLAHI YA BARA LAO

Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki, amewahimiza viongozi wa Bara la Afrika kuwa wakweli na waaminifu katika kulinda maslahi ya bara lao, ili kufanikisha malengo ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Waafrika.

Mheshimiwa Mbeki ameyasema hayo katika hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika tarehe 23 Mei, 2025 jijini Dar es Salaam .

Mheshimiwa Mbeki amesisitiza kuwa maendeleo ya Bara la Afrika yatapatikana endapo viongozi wataweka mbele maslahi ya nchi zao na kuongoza kwa uadilifu, uwazi, na dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya kwa Waafrika wote.

“Tunapoadhimisha Siku ya Afrika mwaka huu kwa kaulimbiu ‘Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia: Kuangazia Historia Yetu, na Kuunda Mustakabali Wetu,’ tunakumbushwa kuwa haki siyo mwisho, bali ni dai endelevu la ukweli, heshima, na uongozi unaoakisi hali halisi za watu wetu. Tuwekeze katika elimu, ubunifu, ushirikishaji wa vijana katika maamuzi, na kupambana na ufisadi unaoharibu maendeleo,” alifafanua Mheshimiwa Mbeki.

Ameongeza kuwa Bara la Afrika lina utajiri na uwezo mkubwa ambao unahitaji Viongozi wanaowaza zaidi ya uchaguzi, wasioogopa uwajibikaji, wenye maono, na wanaotanguliza maslahi ya wananchi wao na Taifa, kuliko matakwa yao binafsi.

Awali Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo alisema kila mwafrika lazima atakafari mafanikio, changamoto na matarajio ya kuinua maendeleo ya Afrika kwa amani ya utulivu.

Amesisitiza umuhimu wa kuwaenzi viongozi walioendeleza fikra za Uafrika na wanaoendelea kupigania ukombozi wa kiuchumi na mshikamano wa Bara la Afrika kwani wameacha urithi mkubwa kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania, nichukue nafasi hii kusema kuwa tunawakumbuka na kuwapongeza waanzilishi wa Umoja wa Afrika (OAU) — ambao ndoto yao ya kuunganisha na kushirikisha zaidi mataifa ya Afrika imeendelea kuishi hadi leo. Tunawakumbuka pia kwa heshima kubwa viongozi waliowafuata, ambao waliendeleza dhima ya Uafrika (Pan-Africanism) na wanaoendelea kupigania ukombozi wa kiuchumi na mshikamano wa bara letu tukufu,” alisema Mhe. Kombo

Hafla hiyo iliwakutanisha pamoja mabalozi , viongozi wa Serikali, Mabalozi wastaafu, viongozi wa serikali, wanadiplomasia, wasomi, pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia na kijamii kwa ajili ya kusherehekea mshikamano, utofauti na maendeleo ya Afrika.

Usiku huo ulipambwa na burudani mbalimbali za kitamaduni, vyakula kutoka nchi za Afrika, pamoja na tafakuri juu ya mchango wa mataifa ya Afrika katika historia na maendeleo ya sasa kuelekea amani na kujitegemea.

Hafla hiyo ilifanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 62 ya Umoja wa Afrika, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa tarehe 25 Mei ya kila mwaka.
.






No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad