HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 30, 2025

MADEREVA 800 WAPATIWA MAFUNZO KUELEKEA MSIMU WA UTALIII

Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi.

KATIKA kuhakikisha msimu wa Utalii (high season) unaoanza hivi karibuni unakuwa katika hali ya amani, Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Arusha limewakutanisha zaidi ya madereva 800 wanaobeba watalii kwa ajili ya kuwapatia mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo pindi wanapotoa huduma hiyo ya usafiri.

Akifungua mafunzo hayo leo Mkoani humo, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP William Mkonda amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha madereva hao sheria na kanuni mbalimbali za usalama barabarani pamoja na kujadiliana changamoto wanazokumbana nazo barabarani ili kuona namna bora ya kuzitatua.

SACP Mkonda amebainisha kuwa Madereva wanaobeba watalii ni watu wa muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa wageni kwani endapo wataendesha magari kwa kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani itapelekea kuitangaza vyema Nchi yetu na hatimaye idadi ya watalii kuongezeka kwa wingi hapa nchini.

Aidha, ametoa wito kwa madereva hao kuhakikisha wanatii na kufuata sheria za usalama barabarani kwa kukosoana, kuelimishana na kuonyana pindi wanapoendesha vyombo hivyo vya moto kwani itasababisha kupunguza au kumaliza ajali zisizokuwa na ulazima barabarani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Waendesha Watalii Nchini (TTGA) Bw. Lembrisi Moses amesema jumla ya madereva 800 wameshiriki katika mafunzo hayo ambapo ameeleza kuwa mafunzo yamewasaidia kuwakumbusha wajibu wao wa kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo alama za barabarani, kuzingatia mwendo sahihi.

Naye Bw. Usia Israel ambaye ni dereva amesema kupitia mafunzo hayo amekumbushwa namna ya kuwa na udereva wa kujihami pindi awapo barabarani ambapo inasaidia kupunguza kero au ajali za barabarani ambazo zinaepukika na kuwataka madereva wenzake kuwa udereva wa kujihami pindi wawapo barabarani.

Mafunzo hayo yamekuja ikiwa ni mkakati wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani katika kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii kwa ajili ya kuwajengea uwezo kuhusiana na sheria mbalimbali za usalama barabarani pamoja na mifumo mipya ya Jeshi la Polisi katika kuwahudumia wananchi.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad