Serikali ya wilaya ya Geita imepanga kutoa jumla ya mifuko 1,071 sawa na tani 53.55 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza na kukamilisha miradi iliyoibuliwa na wananchi kwenye maeneo mbalimbali. Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba alitoa taarifa hiyo akiwa mjini Geita katika hafla ya kukabidhi mifuko 538 ya saruji kwa watendaji na madiwani wa kata zitakazonufaika na mpango huo. Komba alisema saruji hiyo inalenga kuchochea gurudumu la maendeleo kwa kukamilisha majengo ya afya, elimu na ofisi ziliazoanza kujengwa kwa nguvu ya wananchi lakini hazijakamilika. "Saruji ikatumike kwa malengo yaliyokusudiwa. Itasikitisha kama tunakabidhi mifuko ya saruji tukaanza kusikia mifuko ya saruji imeganda", alionya Komba.
Alisema mbali na saruji hiyo, pia ofisi yake imepanga kukutana na wadau wa maendeleo ikiwemo wamiliki wa leseni za madini ili kuwashirikisha namna bora ya kukamilisha miradi ya nguvu za wananchi. “Ndani ya mwezi Juni, kule kote ambako kuna watu wanamiliki leseni za uchimbaji wa madini, na kuna miradi imeshaibuliwa kutakuwa na kikao maalum na madiwani, wenyeviti na wamiliki wa leseni wote.
“Tutajadili miradi ambayo imeibuliwa na wananchi na haijakamilika ili tuwabane pia wamiliki wa leseni wakamilishe wajibu wao wa kurudisha kwa jamii, tusukume pia miradi hii ikamilike kwa wakati" alisema Komba. Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, Lusekelo Mwaikenda alikiri msaada huo ni hamasa kubwa kwa wananchi kuibua na kuanzisha miradi mbalimbali yenye tija kwenye maeneo yao kulingana na uhitaji.
Diwani wa kata ya Bukoli, Faraji Self aliwaomba viongozi wote watakaonufaika na mifuko ya saruji kusimamia kwa weledi ukamilishaji na utekelezaji wa miradi iliyolengwa kwa maslahi ya umma. "Imekuwepo tabia ya kuuza vifaa ambavyo vinatolewa na serikali, au wadau mbalimbali wa maendeleo, tunakwamisha utekelezaji wa ilani, niwaase wananchi ni vyema wakiona watoe taarifa", alisema Faraji.
No comments:
Post a Comment