MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imezindua shindano la Masoko ya Mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu kwa lengo likiwa ni mkakati wa mamlaka hiyo kuongeza uelewa kwa wananchi.
Uzinduzi wa Shindano hilo umefanyika leo Mei 2 mwaka huu jijini Dar es Salaam ,sambamba na kutunuku vyeti kwa wahitimu wa kozi ya watendaji katika Masoko ya mitaji wanaokidhi viwango vya kimataifa.
Akizungumza kuhusu kuzindua shindano la Masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu ,Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA Dk.Nicodemus Mkama amesema katika kutekeleza moja ya mikakati ya Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2019/20 – 2029/30 CMSA inatoa elimu kwa umma kwa lengo la kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi kuhusu fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji.
Dkt.Mkama amesema katika utekelezaji wa mkakati huo CMSA inaendesha Shindano kwa Wanafunzi wa Vyuo vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu kwa lengo la kuongeza uelewa na kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika masoko ya mitaji kwa kutumia njia ya mitandao ya kielektroniki ,yaani simu za mikononi na intaneti.
Ameongeza Shindano hilo linahusisha wanavyuo wa elimu ya juu kote nchini - Bara na Visiwani kushirki na kujifunza kwa vitendo na nadharia fursa mbali mbali za uwekezaji katika masoko ya mitaji.
“Shindano hili tunalozindua leo Mei 2, 2025 linatarajiwa kufungwa Agosti 31, 2025 ili kutoa muda wa kutosha kwa wanafunzi kushiriki bila kuathiri ratiba za masomo. Shindano hili limegawanyika katika sehemu kuu mbili, ambazo ni (shindano la maswali na majibu na Shindano la kuandika Insha -
“Kupitia shindano la Maswali na Majibu (Quiz Competition), wanafunzi wanatakiwa kujibu maswali 100 kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kwa njia ya simu za mkononi, tovuti, na barua pepe, ambapo mshiriki anatakiwa kujisajili kwa kuandika taarifa zake muhimu, ikiwa ni pamoja na majina matatu, jinsia, chuo, na kozi anayosoma, na kisha kufuata maelekezo mengine.
“Kupitia shindano la pili la Kuandika Insha (Essay Competition), Mwanafunzi atatakiwa kuandika insha kuhusu “With practical examples, discuss the role of thematic capital market products in mobilizing resources for financing businesses and development projects”. Insha hiyo inatakiwa isizidi kurasa nne (4), maneno 1,500 na kisha kuituma insha hiyo kwa barua pepe ambayo ni challenge@cmsa.go.tz. “
Amesema Washindi katika mashindano hayo ni wale ambao watapata alama za juu kuliko washiriki wengine na ambao pia wataweza kujibu kwa ufasaha maswali ya usaili utakaofanyika mbele ya jopo la majaji ili kudhihirisha kuwa wao ni washindi.
Dkt.Mkama amesema katika mwaka huu, CMSA imeweka lengo la kuwafikia wanafunzi wapatao 20,000 ikilinganishwa na wanafunzi 18,275 walioshiriki shindano hili mara ya mwisho, ikiwa ni matarajio ya ongezeko la takribani asilimia 10.
“Ili kufikia lengo hili, CMSA imeweka mikakati mbalimbali ya kurahisisha ushiriki wa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano kwa kutumia njia ya simu za mkononi, tovuti, na barua pepe…
“Ambapo mwanafunzi kwa kutumia bando lake la kifurushi cha kawaida ana uwezo wa kuingia kwenye tovuti ya shindano na kupata taarifa na taratibu za ushiriki na kuajiandikasha kushiriki katika shindano la maswali na majibu na hali kadhalika kuwasilisha inshia yake.
“Kwa wanafunzi ambao wako maeneo ambayo yana changamoto za mtandao wa kieletroniki bado wataweza kushiriki shindano hili kwa kutumia barua pepe na simu za mkononi kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi yaani “SMS”. Hivyo basi, wanafunzi wanaweza kutumia simu janja (Smartphone) au kiswaswadu (USSD).
“Ili kuwezesha washiriki wa shindano hili kutumia elimu ya nadharia watakayoipata kwa vitendo, CMSA imeandaa utaratibu wa kuwawezesha washiriki wa shindano hili kuwa wawekezaji halisi. “
Akieleza zaidi amesema kupitia mpango huo washindi 80 watakaopata alama za juu kwenye shindano, watatumia theluthi moja ya zawadi ya fedha taslimu watakazopata ili kuwekeza kwenye masoko ya mitaji kwa kununua hisa na hatifungani za kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam; au vipande katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Mpango huu unatarajia kuongeza wawekezaji wapya katika masoko ya mitaji.
Kuhusu Zawadi zitakazotolewa kwa washindi, Dkt.Mkama amesema washindi wa kwanza kwa kila shindano kwa upande wa wavulana na wasichana watapata shillingi milioni 1.8
Aidha Washindi wa pili kwa kila shindano kwa upande wa wavulana na wasichana watapata shillingi milioni 1.4, Washindi wa tatu kwa kila shindano kwa upande wa wavulana na wasichana watapata shillingi 800,000.
Pia Washindi wa nne kwa kila shindano kwa upande wa wavulana na wasichana watapata shillingi 400,000 na Washiriki waliobaki katika kumi bora watazawadia shilingi 200,000 .
“Washiriki wote waliofika fainali na kuwa miongoni mwa washindi 20 walioshika nafasi za juu watapatiwa vyeti,fulana zenye nembo ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana; na Washiriki 6 wavulana; na 6 wasichana wenye alama za juu zaidi watagharamiwa ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ili kujifunza zaidi maswala ya masoko ya mitaji ikiwa ni pamoja na masoko ya hisa na kampuni kubwa zinazohusika na utoaji huduma katika masoko ya mitaji hapa nchini na nje ya nchi.
Dkt.Mkama amesema pia wanao baadhi ya wanafunzi washindi wa shindano la miaka iliyotangulia, ambao wameweza kuendeleza ndoto zao za kushiriki kwenye soko la mitaji na hivyo kutumia sehemu ya fedha zao walizopata kama zawadi kununua hisa za kampuni mbalimbali zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa.
“Hawa sasa wamekuwa wawekezaji halisi na sio kwa nadharia tu. Nawapongeza sana na kuwaasa muendelee kuweka akiba kwa kuwekeza, kwani ndio njia sahihi ya kutengeneza utajiri utakaowawezesha kuinua kipato na kuboresha maisha yenu.”


No comments:
Post a Comment