HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 19, 2025

Benki ya CRDB Yaadhimisha Miaka 30 kwa Kutoa Jumla ya Gawio Kubwa Zaidi Kuwahi Kutokea la Shilingi Bilioni 170

Arusha 17 Mei 2025 - Katika Mkutano Mkuu wa 30 wa Mwaka wa Wanahisa (AGM) uliofanyika katika kituo cha mikutano cha AICC, wanahisa walikubaliana kwa kauli moja kuidhinisha gawio la Shilingi 65 kwa kila hisa, kiwango cha juu zaidi kuwahi kutolewa katika historia ya benki hiyo. 

Jumla ya gawio lililotangazwa kwa mwaka wa fedha wa 2024 ni Shilingi bilioni 170, ikionyesha uimara wa utendaji wa kifedha wa benki na dhamira yake ya kudumu ya kutoa thamani endelevu kwa wanahisa wake.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, uliofanyika kwa mfumo wa mseto ambapo wanahisa wengine walishiriki kidijitali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, alielezea fahari yake juu ya safari ya mafanikio ya benki hiyo kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita. 

"Tukiadhimisha miaka 30 ya ubora katika huduma za kibenki, gawio hili la kihistoria ni ishara ya uimara wetu wa kifedha na pia ni zawadi ya kipekee kwa wanahisa waliotuamini na kutembea nasi katika safari ya mabadiliko, ubunifu na ukuaji," alisema Dkt. Laay.
Alieleza kuwa gawio la Shilingi 65 kwa hisa, ambalo ni ongezeko la asilimia 30 kutoka mwaka uliopita, linaakisi ongezeko la faida kwa kila hisa hadi kufikia TZS 211.5 kwa mwaka 2024, likichochewa na muundo thabiti wa uendeshaji wa benki, uongozi wa kimkakati na wafanyakazi wenye moyo wa kujituma.

Faida ya Benki ya CRDB baada ya kodi ilikua kwa asilimia 30 hadi kufikia TZS bilioni 551, ikiashiria mafanikio ya mkakati wa muda mrefu wa benki na ufanisi wa uendeshaji. Dkt. Laay pia alizipongeza kampuni tanzu za benki kwa mchango wao unaoongezeka katika mafanikio ya kundi, ambapo kwa pamoja zimetoa mchango wa asilimia 6 katika Faida ya kundi.
CRDB Bank Burundi ilipata faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 40.3, huku CRDB Insurance ikiwa katika mwaka wake wa kwanza wa biashara, ilipata faida ya TZS milioni 343, na hivyo kuimarisha mapato yasiyotokana na riba. 

Wakati huo huo, kampuni tanzu ya Benki ya CRDB DR Congo inaendelea kuonyesha mwelekeo mzuri wa ukuaji na inatarajiwa kufikia kiwango cha faida mapema kuliko ilivyotarajiwa.
Akiwasilisha ripoti yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, alijivunia mafanikio ya miaka 30 ya benki hiyo na kueleza mwelekeo wa miaka ijayo: “Tukiadhimisha miongo mitatu ya kuboresha maisha na kujenga uchumi wa watu wetu na nchi zetu, mafanikio ya mwaka 2024 yanadhihirisha kuwa safari yetu ndio kwanza inaanza. 

Hatua inayofuata ni ya kuleta ushirikishwaji mpana zaidi, mabadiliko ya kidijitali, na athari chanya katika ukanda wetu wa Afrika.”

Nsekela alieleza kuwa mali za benki zimeongezeka hadi kufikia Shilingi trilioni 16.7 (+25.3%), na mkopo wa jumla umefikia Shilingi trilioni 10.4 (+22.7%) kutokana na mikakati inayowalenga wateja na uwezeshaji kupitia mikopo. Benki pia iliongeza upatikanaji wa huduma kwa makundi yaliyosahaulika huduma shirikishi kama akaunti ya Sadaka na mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo kupitia mifumo ya kidijitali.
Alitaja pia ushiriki wa benki katika miradi mikubwa ya kikanda kama vile uwezeshaji wa viwanda vya grafiti kwa kushirikiana na DBSA na IDC, jambo linaloifanya Benki ya CRDB kuwa kichocheo cha ongezeko la thamani na uanzishaji viwanda Afrika Mashariki na Kati.

Uwiano wa gharama na mapato wa benki uliimarika hadi kufikia asilimia 45.7, huku Uwiano wa Mikopo Chechefu (NPL) ukiendelea kuwa chini kwa asilimia 2.9, ikiashiria nidhamu madhubuti ya usimamizi wa gharama na ubora wa mikopo. Uwekezaji katika usanifu wa mfumo wa biashara, uhimilivu wa mtandao na miundombinu ya msingi ya kibenki, umehakikisha uendeshaji thabiti katika mazingira ya kidijitali yanayobadilika kwa kasi.
Nsekela alitoa shukrani kwa wanahisa kwa kuendelea kuiamini benki hiyo, huku akisisitiza maono ya muda mrefu ya benki: “Maadhimisho haya ya miaka 30 ni hatua ya kihistoria. Dira yetu haijabadilika, kuwa taasisi ya kifedha inayoaminika, yenye athari chanya, na tayari kwa siku zijazo kwa vizazi vijavyo.”

Kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, wanahisa waliidhinisha kuteuliwa tena kwa Price Waterhouse Coopers (PwC) kuwa wakaguzi wa nje wa benki kwa mwaka wa fedha wa 2025. Aidha, wanahisa walikubaliana kwamba Mkutano Mkuu wa 31 wa Mwaka ufanyike tarehe 23 Mei 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Mkutano huo pia uliidhinisha kuchaguliwa kwa wajumbe katika makundi yafuatayo:

• Bw. Abdul Ally Mohamed, Bi. Grace Joachim na Dkt. Donald Mmari kuwakilisha wanahisa walio na umiliki chini ya asilimia 1,
• Dkt. Fred Msemwa aliteuliwa tena kuwakilisha wanahisa wenye umiliki kati ya asilimia 1–10
• Na Dkt. Judica King’ori aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Huru.

Akizungumza katika mkutano huo, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mheshimiwa Gelasius Byakanwa, alisifu mageuzi ya benki hiyo: “Benki ya CRDB imekuwa mfano bora wa thamani kwa wanahisa na uadilifu wa kifedha. Rekodi yake ya kutoa gawio kila mwaka na utendaji wake mzuri katika soko la hisa ni ushahidi wa uongozi imara usio na kifani kwa kipindi cha miaka 30.”





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad