HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 24, 2025

WIKI YA WATAALAMU WA MAABARA KANDA YA ZIWA YAZINDULIWA MKOANI GEITA

Maadhimisho ya Wiki ya Wataalamu wa Maabara Kanda ya Ziwa yamezinduliwa rasmi katika Mkoa wa Geita yakilenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa huduma za maabara katika kuboresha afya na matibabu kwa wananchi.
Akizungumza katika Uzinduzi huo uliofanyika katika viwanja vya Kalangalala Manispaa ya Geita Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Omari Sukari amesisitiza dhamira ya serikali kuboresha sekta ya afya kwa kuhakikisha huduma za maabara zinakuwa bora, sahihi na za wakati kwa wananchi.

Amesema zaidi ya shilingi bilioni 97 zimetumika ndani ya miaka minne iliyopita kuboresha miundombinu ya afya mkoani humo, ikiwemo ujenzi wa hospitali za wilaya, Hospitali ya Mkoa na Hospitali ya Kanda Chato.

"Serikali imeimarisha usafirishaji wa sampuli, magari ya wagonjwa ni mapya, na tunaendelea kuwekeza kwenye sekta ya maabara ili huduma za afya ziwe za uhakika. Vipimo sahihi vinamwezesha daktari kumpa mgonjwa dawa sahihi," alisema.

Aidha amewataka watoa huduma katikas sekta ya afya, ikiwemo wataalamu wa maabara, kuwa na leseni  kama takwa la kisheria ili waweze kutoa huduma sahihi na kwa wakati.

Msimamizi wa huduma za maabara katika Hospitali ya Kanda Chato Awadhi Juni amesema kumekuwa na maboresho makubwa katika sekta ya maabara ambapo vifaa na vitendanishi vimeongezeka pamoja na watumishi, hatua iliyosaidia huduma kuwa endelevu na bora.

"Tuna maabara ya kisasa ya kupima vinasaba vya VVU ili kubaini iwapo dawa za kufubaza virusi zinafanya kazi ipasavyo. Pia tumeanzisha huduma ya upimaji wa damu salama ambayo awali haikuwepo Geita, damu ilikuwa ikisafirishwa hadi Mwanza," alisema.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Maabara Kanda ya Ziwa, Joseph Lugala, amesema lengo la wiki hiyo ni kutoa elimu kwa jamii juu ya huduma za maabara, kupima magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, malaria na kuchangia damu.

Pia amesisitiza umuhimu wa kufuata viwango vya ubora katika uchukuaji na uchakataji wa sampuli huku akiiomba serikali kuongeza wataalamu wa maabara kutokana na kada hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa watoa huduma..

Eda Fedinand, mtaalamu wa maabara kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, amesema katika maadhimisho hayao huduma  inatolewa bure kwa wananchi ikiwemo vipimo na ushauri, pamoja na kufanya tafiti kuhusu magonjwa kama kifua kikuu, vidonda vya tumbo na usugu wa dawa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad