UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umetoa wito kwa vijana wa Kitanzania kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mzunguko wa pili wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, unaotarajiwa kuanza Mei 1 hadi Julai 4, 2025.
Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi Taifa wa UVCCM, Jessica Mshama, ametoa wito huo leo Aprili 29, 2025 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Pamoja na wito huo, Jessica ametoa onyo kali kwa watu wanaotaka kuwahadaa au kuwatumia vijana kwa misingi ya kuvuruga amani wakati wa mchakato huu, ikisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani, sheria na utaratibu.
Amesema ushiriki wa vijana katika uchaguzi ni muhimu kwa sababu kundi hilo pia lina asilimia 34.5 ya Watanzania wote kulingana na Sensa ya 2022. “Kila kijana mwenye umri wa miaka 18 au atakayefikisha miaka hiyo ifikapo siku ya uchaguzi mkuu, anatakiwa kuhakikisha amejiandikisha au ameboresha taarifa zake."amesemaa Jessica
Amesema ratiba ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili imegawanywa katika mizunguko mitatu, ambapo mzunguko wa Kwanza kuanzia Mei Mosi hadi Mei 7 katika Mikoa 15 ya Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe.
Mzunguko wa pili utaanza Mei 16 hadi 22, 2025 katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja,
Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.
Pia mzunguko wa Tatu, Vituo vya magereza (130 Tanzania Bara) na vyuo vya mafunzo (10 Zanzibar).
utaanza Juni 28 hadi Julai 04, 2025.
Jessica amesema kuwa kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, jumla ya vituo 7,869 vitatumika katika uboreshaji huo—vikiwemo vituo 7,659 Tanzania Bara na 210 Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Jessica ameeleza kuwa serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kutengeneza zaidi ya ajira milioni nane kupitia sekta za umma na binafsi, sawa na asilimia 115 ya matarajio, kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Reli ya Kisasa ya SGR, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, pamoja na ajira katika sekta za elimu na afya.
"Zaidi ya Sh bilioni 250 zimetolewa kwa makundi ya vijana kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi," alisema.
Jessica amewahimiza vijana kujiandikisha, kuboresha taarifa zao, kuchangamkia fursa za kugombea uongozi na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao.
“Tanzania ya sasa inahitaji viongozi vijana wenye maono, uadilifu na uzalendo wa dhati,” alisisitiza.
Jessica pia alieleza mafanikio mengine ya serikali ikiwemo ongezeko la upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kwa asilimia 77 na mijini kwa asilimia 88. Alitaja pia ujenzi wa shule mpya 3,631 za msingi na sekondari, madarasa 21,912, vituo vya afya 367 na zahanati 980.
Kwa mujibu wa Jessica, vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 huku matumizi ya nishati safi ya kupikia yakiimarika kwa asilimia 85. Pia, huduma ya bima ya afya imeboreshwa na kuwafanya wananchi kupata matibabu kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa.
No comments:
Post a Comment