UJUMBE kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umekamilisha ziara ya siku mbili katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera, kwa lengo la kujifunza uzoefu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika ujenzi na uendeshaji wa miundombinu ya vyuo vya ufundi stadi.
Ziara hiyo ilifanyika kuanzia tarehe 24 hadi 25 Novemba 2024 ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Kuwajengea Uwezo Vijana Kujiajiri na Kuajiriwa kupitia Uchumi wa Bluu (SEBEP).
Ujumbe huo, ukiongozwa na Mhandisi Salumu Mkubwa Abdullah, ulifanya majadiliano na timu ya Tanzania Bara ikihusisha Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Ethel Kasembe, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na timu ya VETA ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, CPA Anthony Kasore. Ujumbe huo pia ulitembelea karakana, majengo na miundombinu mbalimbali ya chuo hicho.
Akizungumza katika majadiliano hayo, Mhandisi Salumu Mkubwa Abdullah amesema, "Tumekuja kujifunza kutoka VETA kwa sababu ya uzoefu wao wa muda mrefu katika ujenzi na uendeshaji wa vyuo vya ufundi stadi na taarifa nyingi tulizozipata kuhusu chuo hiki cha VETA Mkoa wa Kagera. Ni chuo ambacho kimekuwa na sifa nyingi sana.”
Amesema, SEBEP ni mradi wa miaka mitano na utatekelezwa kwa ruzuku ya Sh. Bilioni 125 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ambazo zitatumika katika kujenga vyuo vitano vya mafunzo ya amali, taasisi ya ubaharia, hosteli za wanafunzi wa kike, na karakana za mafunzo ya mafuta na gesi, shabaha ikiwa kunufaisha vijana 43,000.
Kwa upande wake, CPA Anthony Kasore aliipongeza Zanzibar kwa uamuzi wa kujifunza kutoka VETA badala ya kwenda nje ya nchi.
"Mazingira yetu yanafanana, na hivyo kujifunza hapa kuna tija zaidi. Ushirikiano wa muda mrefu kati ya VETA na VTA umekuwa na manufaa, hasa katika nyanja kama uandaaji mitaala na miongozo ya mafunzo,” amesema.
Mawazo ya CPA Kasore yaliungwa mkono na Mhandisi Abdallah Mohamed Hambal, Mkurugenzi wa Vyuo na Mafunzo, VTA akisema kuwa VETA na VTA vimekuwa vikishirikiana katika mambo mengi ya utoaji mafunzo ikiwemo uandaaji mitaala na miongozo mbalimbali ya mafunzo, hivyo suala hilo la kujifunza uzoefu kuhusu ujenzi wa miundombinu linaimarisha ushirikiano zaidi.
Mkurugenzi wa Soko la Ajira, Mipango na Maendeleo, Angelus Ngonyani, alishauri umuhimu wa kuandaa walimu na vifaa vya kufundishia ili kuhakikisha vyuo vipya vinavyotarajiwa vinatoa mafunzo yenye ubora wa hali ya juu.
Amependekeza VETA kupitia Chuo chake cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kuandaa walimu au kuwajengea uwezo ili waweze kutoa mafunzo kwa ufanisi.
Akihitimisha ziara hiyo, Dkt. Ethel Kasembe aliishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuzingatia mabadiliko ya mitaala ili kuendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira na maendeleo ya teknolojia na akahimiza kushirikiana na viwanda katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi.
“Kwa mfano sasa kwa upande wa Tanzania Bara, sasa kuna mpango wa kuongeza ngazi za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Ngazi ya Tatu (Level 3) ya sasa kwenda ngazi ya Nne hadi Shahada ya Uzamivu (PhD) katika ufundi stadi. Ni vizuri pia kuanza kufikiria mabadiliko hayo hata kwa upande wa Zanzibar,” amesema.
Vilevile, amezishauri VETA na VTA kuendelea kuwaelimisha wananchi kuwa mafunzo ya ufundi stadi au mafunzo ya amali si kwa ajili ya walioshindwa, bali ni kwa wale walioona kuwa huku ndio kwenye fursa nzuri ya kuwawezesha kuajirika kwa urahisi na kujikwamua kiuchumi.
Tuesday, November 26, 2024
Home
Unlabelled
SMZ Wachukua Uzoefu wa VETA Kagera katika Ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi
SMZ Wachukua Uzoefu wa VETA Kagera katika Ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment