Benki ya NMB imetoa msaada wa mabati 150 na madawati 150 kwa shule za msingi KASANGA, KISASA na SAWALA zilizopo wilayani Mufindi mkoani Iringa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi millioni 23.
Msaada huo kutoka benki hiyo ni sehemu ya kuunga mkono jithada za serikali katika sekta ya elimu pamoja na kurejesha kwa jamii kama ilivyo utaratibu wa benki hiyo .
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Ndg. Benedicto Baragomwa alisema lengo kubwa la Benki ya NMB ni kuhakikisha inawafikia wateja wake kote nchini kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu.
“Nilikutana na Mbunge wenu wa Mufindi Kusini, Mhe. David Kihenzile akanieleza kuhusu changamoto ya madawati katika shule hii ya Kasanga, Sawala na Kisasa nami nikamuahidi nitafanyia kazi kilio chake na leo kupitia sera yetu ya kurejesha kwa jamii tumewafikia”, alisema Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Ndg. Benedicto Baragomwa.
Baragomwa pia ameziagiza kanda za nyanda za juu kusini za benki hiyo kufanya tathmini ya kina kuhusu uchakavu wa shule mbalimbali na mahitaji ili kusaidia wanafunzi kusoma kwenye mazingira bora .
Aliongeza kuwa Benki ya NMB imepokea ombi la uhitaji wa mabati 110 kutoka Shule ya Msingi Kasanga na wanakwenda kulifanyia kazi ili kuona uwezekano wa kuwapunguzia mzigo wa michango wazazi na walezi .
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameishukuru na kuipongeza Benki ya NMB kwa msaada huo mkubwa ambao unakwenda kuondoa kabisa kadhia ya wanafunzi kuketi chini na hata nyakati zingine kunyeshewa na mvua kwa madarasa kuvuja.
Kihenzile aliwataka wananchi kutumia Benki ya NMB kwa kufungua akaunti mbalimbali ili waweze kujiweka akiba na kuwapa nguvu ya kuendelea kurejesha kwa jamii huku akiipigia chapua benki hiyo kwa kutoa mikopo ya papo hapo kupitia simu ya mkononi.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kasanga akizungumza kwa niaba ya walimu wakuu wa shule zingine zilizopata msaada huo alisema kuwa awali dawati moja lilitumiwa na wanafunzi watano badala ya watatu kama ilivyotakiwa na Wizara ya Elimu lakini sasa msaada huo unakwenda kumaliza kabisa changamoto hiyo.
Nao baadhi ya wazazi na walezi wameahidi kuwa mabalozi wa benki hiyo kwa kuhamasisha wananchi kuitumia ili kuendelea kunufaika na misaada mingine ambayo imeahidiwa na uongozi wa NMB.
Tuesday, November 26, 2024
NMB YATOA MSAADA WA VIFAA VYA SH. MIL. 23 KATIKA SHULE 3 MUFINDI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment