HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 12, 2024

DCEA Yaendelea na Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya: Kilogramu 1,066 Zikamatwa,

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba 2024, na kufanikiwa kukamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 12, 2024 Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), Aretas Lyimo amesema mpaka sasa watuhumiwa 58 wamekamatwa kwenye operesheni hiyo.

"Katika dawa za kulevya tulizozikamata ni pamoja na mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, na tumeweza kuteketeza jumla ya ekari 157.4 za mashamba ya bangi na lita 19,804 za kemikali bashirifu". Amesema Kamishna Lyimo

Aidha amesema kuwa kati ya dawa hizo, kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu moja (01) ya hashishi zilikamatwa eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.

Amesema uchunguzi umebaini kuwa wateja wengi wa skanka ni wanawake, ambao hudai kutumia dawa hizo kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha.

"Skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, inavyosababisha madhara makubwa kiafya. Vilevile, hashishi ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka. Mara nyingi jamii huamini kuwa watu wanaopatwa na magonjwa haya wamerogwa". Amesema

Pamoja na hayo amesema katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Mamlaka ilikamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein, zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi, pamoja na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi.

"Dawa hizi ziliingizwa nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika. Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya, Hali hii inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya na kusababisha wafanyabiashara na watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya". Kamishna Lyimo ameeleza.

Kamishna Lyimo amesema mkoani Dodoma, Mamlaka imewakamata watuhumiwa wawili Suleiman Mbaruku Suleiman (maarufu Nyanda), mwenye umri wa miaka 52, na Kimwaga Msobi Lazaro (miaka 37) wakazi wa mtaa wa Kinyali, kata ya Viwandani.

"Watuhumiwa hao walikamatwa na jumla ya gramu 393 za heroin. Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya mkoani humo na amekuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu". Amesema

Kupitia operesheni za kanda, DCEA pia imekamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin, na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawaomba wananchi waendelee kuunga mkono jitihada hizi kwa kufichua wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara na matumizi ya dawa za kulevya.




























No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad