HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 20, 2024

DAWASA TAASISI YA MFANO UTEKELEZAJI MAAGIZO YA VIONGOZI - DC BULEMBO

-Ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu kufikisha Majisafi Kigamboni_

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Halima Bulembo ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kutekeleza kwa wakati agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa la kutatua changamoto ya ukosefu wa Majisafi kwenye Kata nne za Wilaya ya Kigamboni ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali wa mradi mkubwa wa majisafi wa Kigamboni.

Mhe. Bulembo ameeleza kuwa, mnamo Oktoba 16, 2024, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alitoa maagizo kwa DAWASA ya kuhakikisha Kata za Kisarawe II, Somangila, Kimbiji na Pembamnazi wananchi wanafikiwa na huduma ya Majisafi.

Ameongeza kuwa jitihada kubwa za DAWASA zimeonekana ambapo kazi ya kulaza mabomba ya kusambaza maji sambamba na kutekeleza zoezi la kutambua wananchi wenye uhitaji wa maunganisho ya maji imekwisha kuanza.

"Hizi ni jitihada kubwa na za mfano za kurudi kwa Viongozi na kueleza hatua waliyoifikia katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu," amesema.

Akielezea hatua iliyofikiwa, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa Mamlaka iliitikia agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa la kutatua changamoto ya ukosefu wa majisafi kwenye Kata hizi nne, na kwamba kazi ya kufikisha maji ilishaanza na zoezi la kulaza mabomba ya kusambaza maji kwenye maeneo yaliyoelekezwa ya kihuduma inaendelea.

Ameongeza kuwa, mara baada ya kupokea maelekezo ya Waziri Mkuu, Mamlaka ilifanya tathmini ya kazi nzima na kubaini uhitaji wa ujenzi wa mtandao wa mabomba wa kilomita 221 ya kusambaza majisafi kwenye Kata zote nne, ambapo mpaka sasa jumla ya kilomita 160 za mabomba zimeshalazwa.

"kwa sasa tumebakiza kilomita 60 za kukamilisha katika mwaka huu wa fedha ili wananchi waanze kupata Majisafi na salama," ameeleza Mhandisi Bwire.

"Wito wetu kwa Wananchi wa maeneo haya ni kuwataka wajitokeze kwa wingi ili waweze kuunganishiwa huduma ya majisafi, kwa kuwa Serikali imeshawekeza fedha nyingi ili kila mwananchi apate huduma ya Majisafi," ameeleza Mhandisi Bwire.

Mwakilishi wa Katibu wa CCM Wilaya ya Kigamboni Ndugu Hamza Halfan ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuitikia kilio cha wananchi wa maeneo haya na kutekeleza miradi hii ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa Majisafi. Hii ni hatua nzuri na ya mfano kwa sababu inalenga kutimiza ilani ya Chama ya kuboresha upatikanaji wa maji kwa asilimia 95 kwa wananchi wa mijini.

Nae mkazi wa mtaa wa Mwasonga Bi Hadija Omari ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kumtua ndoo ya maji kichwani kupitia mradi hii. "Jitihada hizi zimeleta faraja kubwa sana kwetu," ameeleza.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad