HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 11, 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI MKUTANO WA JUKWAA LA TASNIA YA KUKU NA NDEGE WAFUGWAO KWA NCHI ZA SADC

 

 

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 17 Octoba, 2024 Serena Hotel jijini Dar Es Salaam.
Akizungumza leo tarehe 11 Oktoba, 2024  jijini Dodoma, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdala Ulega, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe, amesema lengo la mkutano huo ni kukuza fursa za ajira nje na ndani ya nchi pamoja na kujadili na kubadilishana uzoefu wa sekta hiyo  na nchi za SADC.

“mkutano huo utatoa nafasi kwa Tanzania kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo katika Tasnia ya kuku na ndege wafugwao kuongeza wigo wa masoko ya bidhaa hizo katika nchi za SADC na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi za SADC katika Tasnia hiyo” amesema Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe ameshukuru uongozi wa awamu ya sita uliochini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele na kufungua fursa za wawekezaji katika sekta za uzalishaji ikiwemo Tasnia ya Kuku.

Vilevile, Prof. Shemdoe amesema tukio hilo litaambatana na maonesho ya kitaifa ya Tasnia ya kuku na ndege wafugwao yatakayofanyika 18-19 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar Es Salaam.

Prof. Shemdoe amesema, mgeni Rasmi katika mkutano huo ni Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko.

Aidha, Prof. Shemdoe amewakaribisha wadau wote wa ufugaji kuku na watanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika matukio haya, kwani jukwaa hili na maonyesho haya ni bure na hayana gharama zozote.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad