HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 23, 2024

MACHIFU MBEYA WAOMBA ELIMU YA FEDHA IWE ENDELEVU

 


Na Farida Ramadhani na Joseph Mahumi, WF – Mbeya
VIONGOZI wa kimila (Machifu), jijini Mbeya, wameiomba Serikali kuweka program ya elimu ya fedha kuwa endelevu ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata uelewa na kutatua changamoto mbalimbali za masuala ya kifedha.


Wametoa wito huo walipotembelea Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwa mwaka 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe Jijini Mbeya, yaliyobeba kauli mbiu ya “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi”.


Akizungumza kwa niaba ya Machifu hai, Chifu Lyoto, alisema elimu ya fedha ni muhimu kwa kuwa inatoa mwongozo wa namna bora ya kutumia fedha, umuhimu wa uwekaji akiba, mikopo pamoja na namna bora ya kujikwamua kiuchumi.


“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta Maadhimisho haya Mbeya, tunaiomba iendelee kutuletea hii elimu hasa katika maeneo ya vijijini kwa kuwa masuala ya fedha ni muhimu katika maisha yetu”, alisema Chifu Lyoto.


Alisema katika Maadhimisho hayo wamejifunza mengi kuhusu masuala ya fedha na watatumia elimu hiyo kuwaelimisha wengine ambao hawajapata nafasi ya kufika katika viwanja hivyo.


Aidha, aliwakaribisha wananchi wote wa jiji la Mbeya na viunga vyake kutembelea Maadhimisho hayo ili kupata elimu muhimu kwa maendeleo yao na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.


Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21 – 2029/30 ambao pamoja na mambo mengine elimu kwa umma ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango huo.


Maadhimisho hayo yanalenga kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya huduma rasmi za fedha pamoja na kuongeza mchango wa Sekta ya Fedha kwenye ukuaji wa Uchumi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad