HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 16, 2024

Dkt.Biteko :Serikali ,imeweka mazingira wezeshi ya Tasnia ya Ufugaji wa Kuku

*Aiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi ianzishe viwanda vya kusindika vyakula vya kuku.

Na Chalila Kibuda,Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa ujio wa Mkutano wa Jukwaa la Tasnia ya Kuku na ndege wafugwao kwa Nchi za Kusini mwa Afrika unadhihirisha namna Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia ilivyokuwa na mahusiano mazuri katika kufungua fursa kwa watanzania katika kufanya uwekezaji katika sekta ya kuku.

Dkt.Biteko ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Dkt. Philip Mpango katika ufunguzi wa mkutano wa Tasnia ya Kuku na Ndege wafugwao ulioshirikisha nchi 23.

Amesema ufugaji wa kuku na ndege wafugwao una faida katika kuchangia usalama wa chakula na kuongeza pato la Taifa kikanda na kimataifa.

Dkt.Biteko ameilezea mkutano huo kuwa asilimia 55 ya kaya nchini na katika nchi mbalimbali ni ufugaji unaofanywa zaidi na wanawake na vijana na kuwa Tanzania ina kuku milioni 103.1 wakiwemo kuku wa asili na kisasa.

Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha mashamba ya kuku wazazi kwa ajili ya kuzalisha vifaranga, kuanzisha vituo vya kisasa, maabara pamoja na kuwekeza katika machinjio ya kisasa ya kuku.

Dkt. Biteko hata hivyo ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka pia mfumo wa mnyororo baridi wa usambazaji wa kuku pamoja na kuwekeza katika vizimba, chakula cha kuku .

Naibu Waziri Mkuu katika majukumu ya Wizara ianzishe viwanda vya kusindika vyakula vya kuku ili vipatikane ndani ya nchi na sio kutumia fedha za kigeni kuagiza nje.

Dkt.Biteko ametoa wito kwa wadau wote wa ufugaji wa kuku kuendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza majukumu yao kwa kuwa Serikali imetoa fursa kwa kila mmoja kuweza kujishughukisha na kujiongezea kipato.

Dkt. Biteko ameikaribisha sekta binafsi kushiriki katika tasnia hiyo ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi huku akiwataka watafiti kushirikiana na Serikali katika kufanya kazi pamoja.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni matokeo ya mkutano wa AGRA uliofanyika Dar es alaam na kuongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia ambapo AGRA walielezwa juu ya kuipa kipaumbele sekta ya ufugaji wa kuku kwa kuwa nchini Tanzania familia nyingi zinafuga kuku.

“ Tunawashukuru AGRA na Food Alliance kwa kutukubalia na ndio maana leo jukwaa la kwanza limefanyika hapa Tanzania na kutoa fursa kwa wafugaji wetu kujifunza na kujenga mahusiano,” amesema Mhe. Ulega.

Amebainisha kuwa takwimu zinaonesha kuwa ifikapo 2030 tasnia ya kuku itachangia asalimia 41 ya protini na kuwa watafiti nchini.

“ Kuna waatafiti walifanya utafiti kwa kutumia sampuli chache juu ya ulishaji wa kuku wanaofugwa na akina mama na vijana tafiti ile ilileta taharuki, kupitia mkutano huu Naibu Waziri Mkuu utumie fursa ya kueleza hilo kuwaambia watafiti washirikiane na Wizara ili kutotoa taarifa za taharuki kwa jamii na kuwa Serikali inaweza kudhibiti wafugaji wasiofuata taratibu hivyo tusiharibu jitihada zinazofanywa na kukuza tasnia hii inayosaidia wafugaji wetu katika kujipatia kipato na kufanya kuwa ajira” amesema Ulega.

“ Tunawaheshimu na kuthamini kazi zao ila tuone wanapofanya tafiti na kupeleka kwa jamii tuwe na mkakati wa pamoja wa kufikisha tafiti hizo kwa jamii,” amesisitiza Ulega.

Naye, Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia na Mwenyekiti wa Bodi ya Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA), Mhe. Dkt. Hailemariam Dessalegn, amesema kuwa fursa muhimu zilizopo kupitia ufugaji wa kuku ni chanzo cha protini, soko la uhakika na ajira kwa vijana na ka kushiriki katika mnyororo wa thamani.

“Jukwaa hili linatoa fursa ya kujifunza faida na changamoto katika tasnia hii na kuongeza ushirikiano. Kukuza tasnia hii katika nchi yetu inahitaji majukwaa kama haya na inahitaji utayari wa wadau mbalimbali kwa kuwa wana uwezo wa kuwekeza ili kukuza tasnia hii,” amesema Mhe. Dessalegn.

Ameongeza “Tanzania ni kinara wa kuwa na njia shirikishi na ni imani yangu itaendelea hivi chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia ili kufikia ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), haswa dhamira ya kumaliza njaa na umasikini ifikapo 2030. Hakuna nchi inayoweza kufikia mafanikio haya peke yake hivyo sera ya ukanda, mafunzo na majadiliano na mawasiliano ni muhimu kufikia malengo.”

Mfugaji kutoka nchini Malawi, Grace Gondwe amesema kuwa baada ya kumaliza Chuo Kikuu nchini humo alianzisha biashara ya ufugaji wa kuku wa kisasa licha ya kukutana na changamoto mbalimbali amemudu kufanya kazi hiyo kwa miaka mitano sasa na kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha mahitaji yake yaongezeka siku hadi siku.

“ Kupitia ufugaji nimekuwa mshauri pia kupitia Kampuni yangu tumeanza kutumia teknolojia katika uzalishaji wa kuku ambapo uzalishaii umekuwa mkubwa kwa gharama nafuu. Vijana wenzangu napenda kuwaambia tuendelee kufuga kuku kuna fursa nyingi pamoja zinazoendana na ufugaji wa kuku,” amesema Grace.

Mfugaji wa kuku kutoka mkoani Tanga, Bw. Omary Mussa amesema kuwa ameanza ufugaji kupitia miradi mbalimbali na baada ya mafunzo amekuwa mfugaji tangu mwaka 2023 akianza na kuku 500 na sasa anafuga kuku 4,000 aina ya chotara na kuku wa kisasa.

“ Tanzania kufuga kuku ni utamaduni wetu tuna kazi ya kubadilisha kutoka kuwa tamaduni kuwa kibiashara nimeanzisha Kampuni ya Kuku Pesa Investment Group ili watu wafuge kuku kupata pesa,” amesema Mussa.

Ameongeza “ Changamoto ni kuwa watu wanafuga bila faida, Kampuni yetu inatoa mafunzo kwa mtu anaye fuga ikiwa ni pamoja na kubadilisha mitazamo kuwa sio lazima uajiriwe unaweza kujiajiri mwenyewe. Hadi sasa vijana 108 wamepata mafunzo na ufugaji na tuna wafugaji 98 tunaowasimamia mkoani Tanga.”
 

Naibu Waziri Mkuu Dkt.Doto Biteko akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tasnia ya Kuku na Ndege Wafugwao ulioshirikisha nchi 23 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akizungumza kuhusiana na maendeleo ya ufugaji kuku nchini katika Mkutano ulioshirikisha nchi 23  na kufanyika jijini Dar es Salaam.
 

Mkurugenzi  Mkazi wa AGRA Tanzania  Vianery Rwenyendela  akizungumza kuhusiana inavyofanya uwezeshaji wa kwa wafugaji wa kuku katika hatua zote hadi kufika katika masoko,jijini Dar es Salaam
 

Naibu Waziri Mkuu Dkt.Doto Biteko akiwa na vijana ambao wameingia katika ufugaji wa kuku walioshiriki na vijana wanzao walitoka katika mataifa 22 jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad