HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 3, 2024

Benki ya DCB yatenga shs bilioni 30 mikopo ya wafanyabiashara wa masokoni

 



Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mstahiki Songoro Mnyonge, ameipongeza Benki ya Biashara ya DCB, kwa kutenga kiasi cha shs bilioni 30 kwa ajili ya mikopo ya wafanyabiashara ndogo ndogo, wanaoendesha biashara zao katika masoko yaliodhinishwa jijini Dar es Salaam na Dodoma.

Pongezi hizo alizitoa wakati akizindua huduma ya mikopo ya DCB Sokoni, inayowalenga wafanyabiashara wadogo wadogo wanaofanya biashara zao masokoni katika Soko la Magomeni, Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo.

Mstahiki Meya alisema uamuzi wa DCB wa kuamua kutenga kiasi hicho unapaswa kupongezwa kwani unaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha uchumi wa wananchi wa kipato cha chini unaimarika.

“Serikali ilianzisha mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmashauri, mikopo hii haitoshi kuwafikia wajasiriamali wadogo wote ambao ndio kundi kubwa, Halmashauri ya Kinondoni inawaunga mkono na itaendelea kushirikiana nanyi katika kuhakikisha mikopo hii inaleta tija katika masoko mbalimbali yalipo Kinondoni”, alisema Meya Songoro.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Bw. Sabasaba Moshingi alisema uzinduzi wa huduma hiyo unaendana na misingi ya kuanzishwa kwa benki hiyo, miaka 22 iliyopita ambayo ni kuwakomboa kiuchumi wananchi wenye kipato cha chini.

“DCB imeendelea kusimamia vizuri misingi ya kuanzishwa kwake, tokea kuanza kwa huduma hii ya mikopo ya wafanyabiashara wa masokoni, zaidi ya wafanyabiashara 1500 wamenufaika kwa kupata mikopo ya takribani shs bilioni 3 huku tukiwa tumetenga zaidi ya shs bilioni 30 kwa mikopo hii.

“Tunaamini tukishikiriana kwa pamoja, sisi kama benki, serikali, wafanyabiashara na wadau wengine tunaweza kupunguza umasikini kwa kiwango kikubwa.

“DCB tutaendelea kuweka fedha zaidi kwa ajili ya mikopo ya wafanyabiashara, kuongeza nguvu kazi yetu ili tuwafikie wateja wetu mahali walipo, niwapongeze pia wale ambao tayari wamepata mikopo hii kwani mpaka muda huu hakuna mkopo kichefuchefu hata mmoja”, alisema Bw. Moshingi.

Awali akizungumza mahali hapo, Meneja wa Mikopo ya Wajasiriamali, Bi. Sheila Nicas Banzi alisema uzinduzi wa huduma hiyo umelenga kuondoa usumbufu wanaoupata wafanyabiashara hao wanapoenda kukopa katika mikopo kandamizi, maarufu kama ‘Kausha Damu’.

Akizungumza jinsi ya kupata mikopo hiyo, Bi Sheila alisema, sharti muhimu ni kuwa kuwa na kizimba cha biashara katika masoko yaliyoidhishwa na mteja kuwa mwanachama hai wa masoko hayo.

“Mikopo ya DCB Sokoni inatolewa kwa dhamana ya kizimba pamoja na Umoja wa Soko husika kwa kiwango kinachoanzia shs 100,000 hadi shs 1,000,000. Zaidi ya milioni moja kutahitajika dhamana binafsi”, alisema Bi. Sheila.

Mwenyekiti wa Soko la Bw. Daudi Mohamed Dole aliishukuru DCB akisema kuingia kwa benki hiyo sokoni hapo kumewapunguzia uchungu wa tatizo la mitaji na pia muda wa kwenda katika taasisi zenye masharti yasiyo rafiki ya utoaji wa mikopo.

“Wafanyabiashara wa Soko la Magomeni wanakopesheka, tunaishukuru DCB Kwa kutuletea mikopo hii, natoa ushauri kwa wafanyabiashara wa Magomeni na Masoko mengine kuchangamkia fursa hii”, alisema Bw. Dole.

Huduma ya mikopo ya DCB Sokoni imeanzia katika masoko ya Jiji la Dar es Salaam na Dodoma, inatarajiwa pia kupelekwa katika masoko mengine sehemu tofauti.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Songoro Mnyonge (kushoto) akikata utepe kuzindua rasmi huduma ya mkopo uliopewa jina la Sokoni (Sokoni Loan), unaolenga wafanyabiashara wa masokoni katika hafla iliyofanyika katika soko la Magomeni, Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo. (kulia) Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Bw. Sabasaba Moshingi na Meneja Mahusiano Taasisi za Kiserikali wa benki hiyo, Bi. Dalilla Issa (wa pili kulia).

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni , Bw. Songoro Mnyonge, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma ya mkopo uliopewa jina la Sokoni (Sokoni Loan), unaolenga wafanyabiashara wa masokoni uliofanyika katika Soko la Magomeni, Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mkopo wa Sokoni (Sokoni Loan), katika soko la Magomeni, Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo. (kulia) Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Songoro Mnyonge.(kushoto) Meneja wa Mikopo ya Wajasiriamali Wadogo wadogo wa Benki ya DCB, Bi. Sheila Nicas Banzi.

Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Ramadhani Mganga, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mkopo wa Sokoni (Sokoni Loan), a unaolenga wafanyabiashara wa masokoni, katika Soko la Magomeni jijini Dar es Salaam leo.






Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Songoro Mnyonge akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyabiashara mara baada ya uzinduzi rasmi wa mkopo wa Sokoni (Sokoni Loan), uliofanyika katika soko la Magomeni jijini Dar es Salaam leo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad