HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 2, 2024

DKT. POSSI: MENEJIMENTI SHIRIKIANENI, TUISHAURI SERIKALI KUHUSU UENDESHAJI WA MASHAURI YA MADAI NA USULUHISHI

 Wakili MKuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutoa mwelekeo wa Ofisi hiyo kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo Dar es Salaam.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (hayupo pichani) wakati wa kikao cha Menejimenti ya Ofisi hiyo kilichofanyika Dar es Salaam.

Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakimsikiliza Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (hayupo pichani) wakati wa kikao cha Menejimenti ya Ofisi hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam.








DKT. POSSI: MENEJIMENTI SHIRIKIANENI, TUISHAURI SERIKALI KUHUSU UENDESHAJI WA MASHAURI YA MADAI NA USULUHISHI



WAJUMBE wa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) wametakiwa kushirikiana kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao kwa wakati ili kufikia malengo waliyojiwekea ndani ya muda uliopangwa.

Wito huo umetolewa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi wakati wa kikao chake cha kwanza na Menejimenti ya Ofisi hiyo tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Dkt. Possi amesema kuwa malengo ya kikao hicho ni kufahamiana, kuwekana sawa na kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku na kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo, Dar es Salaam.

“Tufanye kazi kwa ushirikiano kwa muda wote, mtu anapokwama apewe ushirikiano, tusing’ang’anie kanuni tu za utumishi, ila haimaanishi tuvunje kanuni na taratibu za Serikali, tupunguze kufuata milolongo isiyo ya lazima ili tuweze kutekeleza majukumu kwa wakati na kubadilika badala ya kufanya kazi kwa mazoea,” amesema Dkt. Possi.

Pia, ameongeza kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imekasimiwa majukumu ya kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake hivyo amewataka wajumbe wa Menejimenti kuishauri Serikali kwa wakati kuhusu uendeshaji wa mashauri mbali mbali ili kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama za uendeshaji wa mashauri na ulipaji wa fidia.

Vile vile ametoa wito kwa menejimenti hiyo kuzingatia mawasiliano kwa kuwa mawasiliano ni muhimu, mawasiliano yafanyike kwa wakati na watoe mrejesho wa hatua za utekelezaji wa majukumu, na wazingatie mnyororo wa kufanya maamuzi kwa kuwa ni muhimu ndani ya Serikali.

Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Alice Mtulo akisoma taarifa ya utekelezaji ya Ofisi hiyo kwa Dkt. Possi ameahidi kumpa ushirikiano na kutekeleza maelekezo na miongozo yote aliyoitoa ili kuongeza tija na ufanisi katika kuhudumia wananchi na kuiwakilisha Serikali na taasisi zake katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi ndani na nje ya nchi.

Dkt. Possi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini, kumteua na kumuapisha kuwa Wakili Mkuu wa Serikali yeye na Bi. Mtulo na wote wako tayari kutekeleza majukumu waliyokasimiwa na Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad