HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 22, 2024

WEKENI TAKWIMU SAHIHI KWENYE MIFUMO KULETA MAGEUZI YA UTENDAJI-MHA WAZIRI


KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Mha. Mwajuma Waziri,akizungumza wakati akifunga Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Usafi wa Mazingira lililoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) jijini Dodoma.



Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile,akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Usafi wa Mazingira lililoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) jijini Dodoma.



SEHEMU ya Washiriki wa Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Usafi wa Mazingira lililoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) jijini Dodoma.

........
* Akemea tabia ya kuweka taarifa zisizoakisi uhalisia
* Aitaka EWURA kusimamia utekelezaji wa miongozo
* Aelekeza Kongamano la Wadau kuwa endelevu

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mha. Mwajuma Waziri, amewataka Watendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira (WSSAs) kuweka taarifa sahihi za huduma ya majii na usafi wa mazingira kwenye mifumo ya taarifa ya MaJIS na NISMS, ili taarifa hizo zisaidie kuimarisha utendaji wa Mamlaka hizo, kujipima na kurahisisha ufuatiliaji wa utoaji huduma kwa wananchi.

Mha. Waziri ametoa maelekezo hayo Agosti 21,2024 jijini Dodoma, alipokuwa akifunga Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Usafi wa Mazingira lililoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

“Ni dhahiri mifumo hii imekuwa ikiisaidia Wizara, EWURA na wadau wengine kupata takwimu kwa urahisi na haraka, hivyo tuhakikishe tunaweka taarifa sahihi ili lengo la kuundwa mifumo hiyo litimie,” alisema.

Mha. Waziri aliipongeza EWURA kwa kuwakutanisha wadau wa usafi wa mazingira nchini kwani kupitia kongamano hilo lililofanyika kwa siku mbili, mipango jumuishi ya usafi wa mazingira itawekwa ili kutatua changamoto za milipuko ya magonjwa kama kipindupindu na kusaidia kuwa na jamii yenye afya bora. Aliitaka Mamlaka hiyo kuendelea kuratibu mikutano ya aina hiyo, kusimamia na kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa miongozo mbalimbali ya usafi wa mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, alisema kongamano hilo limetoa fursa ya wadau wa usafi wa mazingira kushirikiana katika kutafuta suluhu za changamoto zinazoikabili sekta hiyo, matumizi sahihi ya mfumo wa ukusanyaji taarifa, uhifadhi wa takwimu na kujenga uelewa wa pamoja.

“Sisi kama taasisi inayosimamia usafi wa mazingira, tunalichukulia suala hili kwa uzito mkubwa kutokana na umuhimu wake katika kuimarisha afya za Watanzania, tuendelee kushirikiana kuhakikisha azma hii inatimia,” alisema.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wadau kutoka Wizara ya Maji, Wizara ya Nishati, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Maji, Umoja wa Washirika wa Maendeleo ( DPG-WASH), Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na Mamlaka za maji na usafi wa mazingira.

Sheria ya EWURA na Sheria ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, zimeipa EWURA jukumu la kudhibiti kiufundi na kiuchumi sekta za nishati na maji na usafi wa mazingira na kusimamia utendaji wa mamlaka za maji nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad