HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 28, 2024

WANANCHI WA MANYARA WAASWA KUJITOKEZA KUJIANDIKISHA NA KUBORESHA TAARIFA KWENYE DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

Wananchi mkoani Manyara wameaswa kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwakuwa hiyo ni haki yao kisheria.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bi. Giveness Aswile wakati akizungumza katika Kipindi cha Tubonge kinachorushwa na Smile FM ya mkoani Manyara leo tarehe 28 Agosti, 2024 ambapo amewaasa wananchi hao ambao watakuwa na sifa za kuandikishwa kujitokeza mara tu zoezi ka uboreshaji wa Daftari utakapoanza mkoani humo.
"Niwaombe wananchi wa mkoani Manyara wenye sifa za kuandikishwa, wale waliohama au wale wanaoboresha taarifa zao kujitokeza mapema na kutokusubiri siku za mwisho ambazo kwa mazoea huwa na watu wengi" amesema Bi.Aswile.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi, Bi. Saida Hilal amesema kuwa Tume imetoa kipaumbele kwa makundi mbalimbali ya Wazee, wakina mama wenye watoto wachanga wanaonyonyesha (watakaokwenda na watoto wao vituoni), watu wenye ulemavu na wakina mama wajawazito ambao wafikapo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura hawatapanga foleni.
Aidha, Bi. Saida ameongeza kwa kusema kuwa Uboreshaji wa safari hii ni tofauti na ule uliopita huku awamu hii kukiwa na mfumo saidizi wa kuboresha taarifa za mpiga kura kwa njia ya mtandao yaani "Online Voter's Registration System" ambao utamsaidia mpiga kura yule anayeboresha taarifa zake kuanza mchakato huo popote pale alipo kwa kutumia simu janja au kiswaswadu.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unatarajiwa kuanza mkoani Manyara tarehe 4 septemba, 2024 hadi tarehe 10 Septemba, 2024 sambamba na mikoa ya Simiyu na Mara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad