HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 21, 2024

WAKILI MKUU WA SERIKALI AKABIDHIWA OFISI

  

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (aliyesimama kushoto) akipokea nyaraka za makabidhiano kutoka kwa aliyekuwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende mara baada ya kukabidhiwa Ofisi kwenye hafla iliyofanyika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (kushoto) akizungumza na aliyekuwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende muda mfupi kabla ya kukabidhiwa Ofisi kwenye hafla iliyofanyika kwenye Ofisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (aliyesimama katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo mara baada ya kukabidhiwa Ofisi na aliyekuwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende. Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam.

WAKILI Mkuu wa Serikali akabidhiwa Ofisi rasmi tarehe 19 Agosti, 2024 mara baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi amekabidhiwa Ofisi na mtangulizi wake aliyeshika nafasi hiyo, Dkt. Boniphace Luhende. Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe 19 Agosti, 2024 kwenye makao makuu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam kufuatia uteuzi wa Dkt. Ally Possi uliofanyika tarehe 14 Agosti, 2024 kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na kuapishwa tarehe 15 Agosti, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Wewe ni mtangulizi wangu, uliwahi kuongoza Ofisi hii kipindi kilichopita ukiwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na sasa umerejea kuongoza Ofisi hii ukiwa Wakili Mkuu wa Serikali, hapa ni nyumbani, ofisi hii unaifahamu, nikupongeze kwa kuteuliwa na kuaminiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hii, nami niko tayari kukupa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yako,” amesema Dkt. Luhende.

Katika makabidhiano hayo, Dkt. Luhende alimkabidhi Dkt. Possi nyaraka mbali mbali za uendeshaji wa Ofisi ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni sheria mama ya nchi na taarifa ya mashauri yanayoendeshwa na Ofisi hii ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo ya uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi ya ndani na nje ya nchi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake.

Akipokea nyaraka hizo, Dkt. Possi alimshukuru Dkt. Luhende kwa makabidhiano ya Ofisi ili aweze kuendelea kutekeleza majukumu ya Ofisi kwa mujibu wa dhamana waliyokasimiwa na Serikali na amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo na yuko tayari kushirikiana na Menejimenti ya Ofisi hiyo, watumishi na wadau kutekeleza majukumu ya Ofisi kwa niaba ya Serikali katika kuhudumia wananchi.

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo ambaye amewapongeza viongozi hao na kuwatakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu kwa kila mmoja kwa nafasi yake katika kuendeleza gurudumu la maendeleo.

Prisca J. Ulomi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad