Na Mwandishi Wetu,Tabora
Kampuni ya ununuzi wa Tumbaku ya Alliance One imeanza kuchukua hatua za kurejesha misitu ya asili iliyoharibiwa na shughuli za kibinadamu kwa kupanda miti 1,062,500 katika mradi wa shamba la miti la Ngukumo wilaya ya Nzega mkoani Tabora wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 980.
Akiongea mbele ya ugeni wa mbio za Mwenge uliotembelea shamba hilo, Msimamizi Mkuu wa Misitu wa Kampuni hiyo, Rashid Salum amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa mkakati wa Kampuni ya Alliance One ya kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya kunakozalishwa tumbaku, ambapo walianzia Kasulu mkoa wa Kigoma mwaka 2014 ambako waliopanda miti katika hekta 450.
“Baada ya kuona mkoa wa Tabora una tatizo kubwa la uharibifu wa misitu kutokana na kukata miti ya kukaushia Tumbaku, mkaa na kuni tuliamua kutafuta eneo katika wilaya ya Nzega na Halmashauri ikatupatia eneo ambalo tumepata hekta 469 zenye vitalu vitano vyenye jumla ya miti,” amesema Salum.
Amesema Kampuni ya Alliance One iliingia mkataba wa makubaliano na Halmashauri ya wilaya ya Nzega kuanzisha mradi wa upandaji miti kwa umiliki kwa mkataba wa Alliance One kumiliki asilimia 80 na Halmashauri ya Nzega kumiliki asilimia 20. Alisema mradi ulianza rasmi Desemba 2022/23 kwa kusafisha eneo, kuchimba mashimo na kupanda miti aina ya Mfudufudu au Mitiki Myeupe, ambayo kupandwa hadi kuanza kuvunwa inachukua miaka saba.
Amesema Kampuni ya Alliance One ina programu tatu za uzalishaji miti ambapo ya kwanza wanawahamasisha wakulima wenyewe kupanda miti katika maeneo yao(Farmer Planting) kwa ajili ya kukaushia tumbaku badala ya kukata miti ya asili ambayo kwa sehemu kubwa imesababisha uharibifu wa misitu.
Programu ya pili ni(Community commercial) wakulima wanapandiwa miti na Kampuni kwa kuwagharamia mpaka asilimia 40 katika mashamba ya pamoja na program ya tatu ni ile ya (Joint forest Management) ambayo Kampuni yenyewe inaanzisha shamba na kupanda miti kama lile la Ngukumo wilayani Nzega.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru mwaka huu Godfrey Mnzava aliongea kwenye hafla hiyo ya kutembelea shamba hilo amesema ili shughuli za kilimo cha tumbaku ziweze kuwa endelevu ni lazima ziende sambamba na upandaji miti ya kukaushia zao hilo.
“Mwenge uhuru unayamulika makampuni yote ya tumbaku nchini na kuwaasa wapande miti na pia tunawashauri wahimize wakulima wao kufanya, hivyo ili kusaidia kutunza mazingira na rejesha ukijani unaopotea kutokana na kilimo cha tumbaku pamoja na shughuli zingine za kibinadamu,”amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega, Afisa Mtendaji wa Kata ya Nkiniziwa Maria Katema amesema shamba hilo litarejesha misitu iliyoharibiwa na shughuli za kibinadamu katika wilaya hiyo.
Katema amesema eneo lililopandwa miti na Kampuni ya Alliance One, hapo awali lilikuwa msitu mkubwa, lakini uliharibiwa na shughuli za kibinadamu zikiwemo cha kutengeneza mkaa, kuni za kukaushia Tumbaku, Kilimo na kulishia mifugo hali iliyotishia kuwa jangwa.
“Pamoja na kutarajia kupata miti baada ya miaka saba, lakini pia mradi huo umeleta ajira kwa zaidi ya Wananchi 300 kutoka katika maeneo mbali mbali ya Kata hiyo wanaoajiriwa kwa kazi za kusafisha eneo, kupalilia na kutunza miti” Alisema Katema
Ametoa onyo kwa wanaojaribu kuharibu shamba hilo kwa kuingiza mifugo ama kufanya shughuli za kibinadamu na kwamba atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
Amewataka viongozi wa Serikali za vijiji, vitongoji na Wataalam wa miti wa Kampuni ya Alliance kuendelea kutoa elimu ili Wananchi wapate uelewa wa umuhimu wa kupanda miti, kutunza na kuilinda kwa faida yao na vizazi vijavyo.
Naye Mkazi wa Kijiji hicho Mzee Joseph Mshine ameipongeza Kampuni ya Alliance One kwa kuanzisha shamba la miti katika eneo lao ambalo lilishapoteza uoto wa asili kutokana na uharibifu wa mazingira na amewaasa Wananchi wenzake kutoka ingiza mifugo katika shamba hilo huku akiiomba Kampuni hiyo kupanua wigo zaidi wa kupanda miti. Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mzava akitoa neno wakati msafara wake ulipotembelea shamba la miti lililopo Kijiji cha Ngukumo kata ya Ikinizwa wilayani Nzega,Mkoani Tabora.Shamba hilo limepandwa na linatunzwa na Kampuni ya Alliance One kwa ajili ya matumizi ya wananchi.
Msimamizi wa Misitu wa Kampuni ya Allaice One akimkabidhi risala fupi ya shamba la misitu liliopandwa na kampuni hiyo kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa Nzega kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka huu Godfrey Mzava wakati msafara huo ulipotembelea shamba hilo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mzava(Katikati) akikata upete kwenye shamba la miti lililopo Kijiji cha Ngukumo kata ya Nkikizwa wilayani Nzega,Mkoani Tabora, wakati msafara wa Mwenge ulipotembelea shamba hilo lililopandwa na kutunzwa na Kampuni ya Alliance One kwa ajili ya matumizi ya wananchi. Baadhi ya wanaoshuhudia tukio hilo ni Msimamizi wa Miti wa Kampuni hiyo Salum Rashid(Wa tano kulia) na Mbunge wa Nzega Vijijini Hamis Kigwangallah(mwenye shati la Kijani)
No comments:
Post a Comment