Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeiongezea bajeti Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Wilaya ya Busega iliyopo mkoani Simiyu kutoka shilingi milioni 500 hadi shilingi bilioni 2.4.
Hayo yameelezwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Busega, Mhandisi Mathias Mgolozi mapema wiki hii.
“Miaka minne iliyopita wilaya ya Busega ilikuwa na bajeti ya shilingi milioni 500 kwa mwaka, baada ya kuingia madarakani Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan bajeti ya TARURA wilaya ya Busega imepanda kutoka milioni 500 hadi bilioni 2.4 kwa nyongeza ya tozo bilioni 1.2, mfuko wa jimbo milioni 500, na mfuko wa barabara milioni 748 na kufanya jumla ya bilioni 2.4,” amesema Mhandisi Mgolozi.
Amesema, kutokana na nyongeza hiyo, TARURA imekuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi nyingi, ambapo kwa mwaka 2023/24 wametengeneza kilomita 100 kati ya kilomita 511 walizonazo kwenye mtandao wa barabara wilayani humo.
Ametaja miradi waliyotekeleza kuwa ni ujenzi wa daraja la Mwamanyili lenye upana wa mita 20 kwa gharama ya shilingi milioni 121.6; barabara ya Mwamigongwa kwenda Nyaluhande yenye urefu wa kilomita 6 pamoja na kufungua barabara mpya zenye urefu wa kilomita 4.8 kwa gharama ya shilingi milioni 237.
Miradi mingine iliyotekelezwa ni ujenzi wa madaraja matatu ya Mwamigongwa yenye upana wa mita 12, mita 8 na mita 6 kwa gharama ya shilingi milioni 477.
“Kwa bajeti ya zamani ya milioni 500 ina maana tungejenga madaraja haya matatu tu kwa mwaka mmoja, lakini kwa nyongeza ya hii bajeti imetuwezesha kufanya kazi nyingi,” amesema Mhandisi Mgolozi.
Naye, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nyaluhande, Robert Mabeyo amesema kwa mara ya kwanza ameona barabara zenye zaidi ya miaka 50 zikijengwa na TARURA kijijini hapo.
“Nina umri wa miaka 50 sijawahi kuona hii barabara ikitengenezwa, lakini ndani ya uongozi wa Rais Samia tumetengenezewa barabara hii ya Nyaluhande,” amesema Bwana Mabeyo
Wilaya ya Busega inaundwa na kata 15, TARURA wilaya ya Busega inahudumia barabara zenye urefu wa kilomita 511.10, na ina jumla ya barabara 136.
No comments:
Post a Comment