HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 3, 2024

Ujenzi wa nyumba za wananchi waliokumbwa na mafuriko Hanang wafika hatua nzuri

 


Muonekano wa baadhi ya Nyumba zilizojengwa na Serikali kwa wananchi waliokumbwa na maafa ya Maporomoko ya Matope na Mawe Hanang zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.


Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amewapongeza SUMA JKT kwa hatua nzuri waliyofikia katika Ujenzi wa Nyumba za Makazi kwa wananchi waliokumbwa na Mafuriko ya Mawe na Matope mwezi Disemba Mwaka Jana.

Waziri ametoa Kauli hiyo wakati alipotembelea na kujionea maendeleo ya Ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa katika eneo la Waret, katika Kijijiji cha Gidagamowd kata ya Mogitu wilaya ya Hanang’ leo tarehe 02/072024.

Ujenzi wa nyumba hizi ni kielelezo cha dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya uzalendo kwa Taifa lake, utu na mapenzi kwa wananchi katika kuwatumikia.

“Nimefurahi mmerithisha ujuzi wa ujenzi kwa sababu nyumba hizi zimejengwa kwa ubora wa hali ya juu na kuzingatia kanuni za kiuhandisi wakati wa ujenzi,” alisema Waziri Mhagama.

Aidha ameelekeza kwa uongozi wa Mkoa wa Manyara kuhakikisha miundo mbinu ya Elimu, Soko na Afya inakamilika kwa muda unaotakiwa kama ilivyofanywa katika urejeshaji wa hali kwa kuhakikisha huduma za maji, nishati ya umeme inapatikana sambamba na ufunguaji wa barabara.

Waziri Mhagama amesema, “Makazi yanapendeza na baada ya muda Mji huu utakuwa Mkubwa sana na utakuwa Mji wa kihistoria ni vyema tukaendelea kutuna mazingira ili kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi.”

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ Mhe. Halimish Issa Hazali amesema Waziri Mhagama ametembelea Nyumba za SUMA JKT nyumba 73 na 1 UWT na ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi na pia ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa nyumba 35 zinazosimamiwa shirika la Msalaba Mwekundu.

Nimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya na anaendelea kuifanya kwa wananchi wa Hanang.

Awali Kaimu Kamanda wa Ujenzi wa Nyumba Luteni Kanali Ashiraf Hassan amesema wamefarijika kwa ziara ya Waziri Mhagama na wamejipanga kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

“Hatuwezi kumuangusha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika adhima yake ya kuhakikisha anawapatia wananchi wa Hanang waliokumbwa na Mafuriko ya Matope na Mawe nyumba bora,” alisema Kaimu Kamanda wa Ujenzi Luteni kanali Hassan.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad