HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 13, 2024

VIONGOZI VYAMA VYA SIASA WAKUMBUSHWA KUSOMA SHERIA YA TUME HURU YA UCHANGUZI


WAKATI vyama vya siasa vikiitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), isimamie uchaguzi wa serikali za mitaa, tume hiyo imevishauri vyama hivyo vikasome Kifungu cha 10 (1) (C) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ili viache kupotosha wananchi.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima wakati akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza kwa waandishi wa habari 250 leo jijini Dar es Salaam.

Kailima amesema kumekuwa na muendelezo wa viongozi wa vyama vya siasa kuitaka INEC isimamie uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa hoja kwamba Sheria ya Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi inataka hivyo, jambo ambalo sio kweli.

"Waandishi wa habari nyie ni watu muhimu sana kwenye mchakato wote wa uchaguzi, sisi INEC, wanasiasa na wananchi wanawategemea mtoe bahari zenye usahihi, naomba hili la wanasiasa kutaka sisi tusimamie uchaguzi mliandike kwa usahihi kwani kwa sheria iliyopo sasa hatuna mamlaka hiyo hadi Sheria itungwe na Bunge.

Kifungu namba 10(1)(c) kinasema kwa kuzingatia matakwa ya Ibada za 74(6), 75 na 78 ya Katiba, Tume itakuwa na majukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za vijijini, mitaa na vitongoji Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika Sheria itakayotungwa na Bunge," amesema.

Mkurugenzi huyo amesema pamoja na kifungu hicho wanasiasa wameamua kupotosha, hivyo kuwaomba waandishi wa habari kutumia taaluma yao kueleza ukweli ili jamii isipotoshwe.

Akizungumzia uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Kailima amesema zoezi hilo linaendeshwa kwa Kifungu 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba moja ya mwaka 2024, Kifungu cha 10(1)(a) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi namba mbili ya mwaka 2024.

Pia amesema masharti ya vifungu rejewa yanaitaka INEC kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili kati ya uchaguzi mkuu uliomalizika na kabla ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi mwingine na masharti ya Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Kailima amesema katika kutekeleza sheria na masharti hayo wanatarajia kuandikisha wapiga kura wapya milioni 5, 586,433 sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura milioni 29,754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika 2019/20, huku wapiga kura milioni 4,369,531 wakitarajiwa kuboreshewa taarifa zao.

"Wapiga kura 594,494 2 wanatarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye daftari, hivyo baada ya uboreshaji INEC inatarajia kuwepo wapiga kura milioni 34, 746,638," amesema.

Mkurugenzi huyo amesema kutakuwa na vituo 40,126 vya kuandikisha wapiga kura ambapo vituo 39,709 vitakuwa Tanzania Bara na 417 Zanzibar ikiwa ni ongezeko la vituo 2,312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika mwaka 2019/20.

Aidha, Kailima amesema INEC imeweka mifumo ambayo inaruhusu Watanzania wenye sifa na wanaomiliki simu janja kuanzisha mchakato wa kujiandikisha au kuboresha taarifa zake kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Amesema mkakati wa INEC ni kuona wananchi wanaotumia simu ambazo sio janja yaani jina maarufu Viswaswadu nao kuanza kufanya mchakato wa kujiandikisha kabla ya kufika kwenye kituo cha kujiandikisha kumalizia zoenzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa INEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jocobs Mwambegele amewataka waandishi kutumia kalamu zao kutoa elimu ya mpiga kura, ili kila mwananchi aweze kushiriki uchaguzi.

"Tumewaita hapa kwa sababu ili haya ambayo tunafanya yaonekana kalamu zenu ndio zinaweza kuonesha kwamba INEC na wadau wake wanafanya kazi, hivyo tunaomba msikubali kupotosha jamii, simamieni taaluma zenu," amesema.

Mwenyekiti huyo amewataka wananchi kutumia kituo cha kutoa huduma, pale ambapo watakuwa na changamoto za uandikishaji au uboreshaji wa taarifa zao.

Naye Mjumbe INEC, Jaji Asina Omari amesisitiza kuwa ufanisi wa tume hiyo utaonekana kupitia vyombo vya habari na kuwataka waandishi kushirikiana nao ili lengo la kuwa na uchaguzi wenye tija liweze kufanikiwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad