HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 18, 2024

TANZANIA YAZINDUA MKAKATI WA KUJENGA MAJENGO YA BALOZI ZAKE NJE NA VITEGA UCHUMI KUONGEZA MAPATO NCHINI

 

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua ujenzi wa Majengo Pacha ya ghorofa 22 kila moja jijini Nairobi, Kenya, yatakayotumika kama Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya na kitega uchumi ili kuongeza fedha za kigeni nchini.

Katika uzinduzi huo uliofanyika katika eneo la kibiashara la Upper Hill jijini Nairobi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba, amesema majengo hayo ambayo ujenzi wake utagharamiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), yataipa Tanzania fursa ya kutumia eneo ililonalo Kenya kujenga ubalozi na kupangisha kwa makazi na ofisi eneo hilo ili kupata fedha.

Mhe. Waziri Makamba ameeleza kuwa, Tanzania inatumia kiasi cha shilingi bilioni 29 kwa mwaka kulipa kodi kwa ajili ya balozi na makazi ya watumishi wake wanaofanya kazi nje ya nchi na kwamba ujenzi huu ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kutumia viwanja na majengo yake ili kuongeza mapato ya nchi.

“Kwa sasa kwa mwaka tunatumia wastani wa shilingi bilioni 29 kulipa gharama za kupangisha ofisi zetu za kibalozi na nyumba za mabalozi wetu duniani kote. Kupitia mkakati huu mpya ambao unaanzia Kenya, tumepanga kuanza kuingiza zaidi ya shilingi bilioni 36 kwa mwaka kupitia uwekezaji tutakaofanya kwenye majengo na viwanja vyetu vilivyopo ughaibuni.

Tanzania itajenga majengo hayo kwenye eneo ililopewa bure na Serikali ya Kenya kwa ajili ya kujenga ubalozi wake – ikijibu ukarimu wa namna hiyo uliofanywa na Tanzania kwa kuipa Kenya bure eneo ambako imejenga ofisi za ubalozi wake, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Eneo hilo ambalo Tanzania imepewa kujenga ubalozi wake, ni mojawapo ya maeneo ya kimkakati jijini Nairobi, kukiwa na ofisi nyingi za serikali huku ikiwa inatazamana na ulipo ubalozi wa Uingereza katika taifa hilo.

Akizungumza katika tukio hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Mhe. Deo Ndejembi, alisema uamuzi wa kujenga majengo hayo ulizingatia upembuzi yakinifu uliofanywa na wataalamu na kuona namna mradi utakavyoingiza mapato kwa serikali.

“ NSSF ina Kamati ya Uwekezaji ambayo kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi na wataalamu wetu wa masuala ya uwekezaji waliutazama mradi huu na kuona utakuwa na faida kwa nchi yetu. Kwa sasa, mwelekeo wetu ni kutazama miradi yenye faida na maslahi kwa taifa,” alisema Ndejembi.

Kwa sasa, ubalozi wa Tanzania nchini Kenya unafanya shughuli zake katika ghorofa ya tisa ya jengo la Re Insurance jijini Nairobi ambako serikali inalipa kodi ya pango kwa ubalozi na inalipia pia kodi za pango kwa watumishi wake wanaoishi nchini humo.

Mgeni rasmi katika tukio hilo, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Musalia Mudavadi, alipongeza hatua ya Tanzania kujenga jengo hilo akisema litakuwa mojawapo ya alama za kudumu za uhusiano wa kirafiki baina ya nchi hizo mbili.

“ Nimeona ramani na picha jongefu za majengo haya zitakavyokuwa. Nimependa ubunifu wa majengo pacha kwa sababu tutakuwa tukiona, tutakumbuka kwamba Tanzania na Kenya ni pacha kwenye uhusiano,” alisema.

Mudavadi ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha wa Kenya, alisema serikali yao pia imejifunza kitu kuhusu namna ya kutumia fedha za taasisi kama NSSF kwa kufanya uwekezaji ili zizalishe zaidi na kuwa muda si mrefu, Kenya itafuata nyayo za Tanzania kwenye utaratibu huo.

Kwa ujumla, Tanzania ina jumla ya majengo 109 na viwanja 11 duniani kote – na kwa mujibu wa mkakati mpya uliopitishwa na Wizara ya Mambo ya Nje hivi karibuni, lengo la serikali ni kutaka kuona inatumia mali zake hizo kuingizia nchi mapato.

Imetolewa na:

 

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad