


Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Kambi ya kampeni ya Dk. Samia,Dr.Peter Kyamba, leo akimweleza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela,mafanikio makubwa ya upasuaji uliofanywa na madaktari hao katika hospitali ya wilaya hiyo.
Picha zote na Baltazar Mashaka
NA BALTAZAR MASHAKA,ILEMELA
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu,amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,kwa kuona umuhimu mkubwa wa kuwasogezea karibu huduma za kibingwa wananchi wasio na uwezo kiuchumi.
Alitoa kauli hiyo leo alipotembelea kambi ya madaktari bingwa wa Dk.Samia,katika Hospitali ya Wilaya ya Ilemela,katika Mtaa wa Isanzu,Kata ya Sangabuye,kujionea huduma za kibingwa zinavyotolewa kwa ubora na kusababisha ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma za afya na ushauri wa kitaalamu.
Wayayu amesema kambi hiyo ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali,imeleta tija na ufanisi na kuwawezesha kwa vitendo madaktari wenyeji namna bora ya kuwahudumia wananchi kwa kutumia vifaa vya kisasa vilivyopo hospitalini hapo.
Amesema,madaktari bingwa hao pia wametoa maoni na mapendekezo ya aina ya vifaa na huduma zinazopswa kuongezwa zaidi katika kuongeza ufanisi na tija katika utendaji na utoaji huduma za afya kwa wagonjwa wanaohudumiwa katika hospitali hiyo.
“Kipekee nitumie fursa hii kumshukuru Rais Dk.Samia kwa maono yake na kuona umuhimu mkubwa kuwasogezea wananchi wa kawaida huduma hizo za matibabu ya kibingwa,ukizingatia wengi wao hawana uwezo wa kiuchumi wa kumudu gharama za kuwaona madaktari bingwa wa magonjwa yanayokabili,”amesema Wayayu.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya kambi hiyo,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Ilemela,Dr.Mateso Mayunga amesema huduma za kibingwa za magonjwa ya watoto,wanawake,upasuaji,magonjwa ya ndani na huduma za usingizi na ganzi salama zinaendelea kutolewa.
“Hadi sasa wagonjwa 140 wamehudumiwa ikiwa ni zaidi ya asilimia 100 ya wagonjwa wanaohudumiwa kwa siku katika hospitali yetu sambamba na makusanyo ya sh.milioni 1.3 kwa siku nne za uwepo wa madaktari bingwa,”amesema Dr.Mayunga.
“Tumefanikiwa kufanya operesheni mbili kwa mafanikio makubwa,sisiti kusema hospitali hii inaweza kufanya makubwa zaidi ya haya kikubwa ni kubuni mbinu za namna ya kuwavutia wateja kwa kuboresha utoaji wa huduma zake,” amesema Dr.Peter Kyamba bingwa wa upasuaji.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani, Dr.Irene Makundi amewasahuri wananchi kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kufuatilia kwa karibu afya zao kwa sababu inaonyesha wengi wao ni wagonjwa lakini hawana ufahamu (hawajijui).
“Kwa siku nne nimekuwepo hapa wagonjwa wengi wana shida ya shinikizo la damu,wanatembea likiwa juu sana wengine likiwa chini na wanaendelea na shughuli zao, hali hiyo ni hatari kiafya,” ametahadharisha Dr.Makundi.
Aidha Madaktari hao wamesifu mazingira ya usafi yaliyopo hospitalini hapo huku wakipongeza watumishi kwa namna wanavyofanya kazi za kuwahudumia wagonjwa kwa weledi na ukarimu.
No comments:
Post a Comment