HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 28, 2024

AIR TANZANIA KUONGEZA SAFARI ZA KIMATAIFA,KUPASUA ANGA HADI OMAN

  

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania,Mhandisi. Ladislaus Matindi akimkabidhi Balozi wa Oman nchini hapa,Balozi Saud bin Hilal Alshaidani (kulia), Jarida la Twiga linalotumika ndani ya ndege za ATCL baada ya mazungumzo kuhusu kuanzisha safari za Oman.
Picha kwa hisani ya ATCL
Balozi wa Oman nchini hapa,Saud bin Hilal Alshaidani (kulia)akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania,Mhandisi Ladislaus Matindi namna wanavyoweza kushirikiana kibiashara kwa nchi hizo mbili.

NA BALTAZAR MASHAKA
KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL),katika kutanua wigo wa safari zake za kimataifa, inajiandaa kuanzisha safari za moja kwa moja kuelekea Muscat,nchini Oman amesema Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi baada ya kukutana na Balozi wa Oman nchini,Saud bin Hilal Alshaidani mapema Juni 26, mwaka huu katika Ofisi za Ubalozi wa Oman,jijini Dar es Salaam.

"Taratibu za kufungua kituo nchini Oman zimeanza na tayari Air Tanzania tumeshampata wakala mkuu wa mauzo (General Sales Agent)ya tiketi nchini Oman na tumeteua msimamizi wa kituo hicho,"amesema.

Mhandisi Matindi amesema hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kukamilisha uandaaji wa timu ya marubani na ndege itakayotumika pamoja mpangilio wa safari hizo za Oman.

Naye Balozi wa Oman nchini Tanzania,Saud bin Hilal Alshaidani amesema mazungumzo yake na Air Tanzania yamekuwa na tija ambapo wamejadili fursa zilizopo kwa kutumia ndege za abiria na mizigo.

"Kwa idadi kubwa ya raia wa Oman waliopo nchini hapa,biashara kati ya nchi hizi mbili ikiendelea kukuzwa,ni matarajio yangu Air Tanzania itanufaika na fursa hii pasi na mshindani bali mshirika kwa upande wa abiria na mizigo",amesema Balozi Alshaidani na kuyataja mazao matatu (maembe,nanasi na parachichi) ya kutiliwa msisitizo.

Balozi huyo wa Oman nchini ameongeza kuwa; “Tunaweza kujikita kwenye usafirisha aina tatu tu za matunda zenye uhitaji mkubwa nchini Oman.Hii itanufaisha pande zote mbili,wafanyabiashara wa Tanzania na Oman.”

Kwa sasa Air Tanzania inafanya safari za ndani na nje ya nchi,kikanda na kimataifa na safari za Dubai (UAE),Mumbai (India),Guangzhou(China),Bujumbura (Burundi),Entebbe(Uganda),Hahaya (Comoro), Harare (Zimbabwe),Lusaka na Ndola (Zambia),Nairobi (Kenya) na Lubumbashi (Congo).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad