HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 29, 2024

TGNP YAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA HABARI

Na Mwandishi wetu

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), unatoa mafunzo kwa waandishi wa habari 24 kutoka vyombo vya habari ngazi ya kijamii ambayo yamelenga kuongeza uelewa na uwezo kwa waandishi hao ili waweze kutambua nafasi zao katika jamii.

Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika Ofisi ya TGNP jijini Dar es salaam Leo Mei 29, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi amesema mafunzo hayo yamehusisha waandishi wa habari kutoka Mikoa ya Morogoro, Manyara na Kilimanjaro.

Amesema mafunzo hayo yatajikita katika maeneo matatu ambayo ni kujifunza mbinu za kuandika na kuripoti habari zenye athari chanya katika jamii yetu ambapo wanajifunza namna ya kuandika kwa njia inayobadilisha mitazamo hasi na kuleta mabadiliko ya kweli.
 
Amesema mafunzo hayo yanajikita katika kupitia mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii yetu ambapo tutajifunza jinsi ya kuandika habari zinazochangia katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kuhamasisha mabadiliko ya kimfumo na kitamaduni.
 
Vilevile mafunzo hayo yatatuwezesha kujadili kwa kina jinsi ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ambapo tutachambua changamoto na fursa zinazowakabili wanawake katika kujitokeza na kushika nafasi za maamuzi katika jamii yetu.
 
Liundi amesema eneo lingine ni kuhusu mradi wa wanawake vijijini waletao mabadiliko (RWCC) ambapo waandishi hao wataweza kuangalia umuhimu wa kilimo ikolojia na namna vyombo vya habari ngazi ya jamii vinaweza kuhamasisha wanawake zaidi kushiriki katika kilimo hicho pamoja na kukipa uzito katika jamii.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema mafunzo hayo yamekuja kwenye wakati muafaka tukielekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mtaa.

"Hawa wanawake wakulima wadogo wadogo wa vijijini tunafahamu wananafasi kubwa ya kushika nafasi za maamuzi katika uchaguzi huu hivyo waandishi wa habari wa vyombo vya ngazi ya jamii mnaweza kuhamasisha wanawake wakulima wadogo wadogo wa vijijini kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za mtaa,"amesema Liundi.

Aidha amesema mafunzo hayo yatatoa fursa ya kuangalia hali halisi na kuangalia fursa zilizopo na namna gani waandishi habari wanaweza kufanya kuhakikisha wanawake wanapata habari zaidi na kugombea nafasi hizo.

Akizungumzia kuhusu kilimo ikolojia Liundi amesema kilimo hicho kinafaida ni cha asilia kwasababu hakitumii dawa.

"Kilimo hiki kinatumia mbolea za asili na ni kilimo cha afya zaidi na wanawake wengi wa vijijini wamekuwa wakikitumia,"amesema Liundi.

Amesema kuwa Serikali ya Tanzania imeweza kutambua kwa kiwango fulani kuhusu kilimo hicho na kuna juhudi ambazo zimekuwa zikifanyika .

Akitolea mfano amesema Serikali imeanzisha Idara ya kilimo ikolojia katika Wizara ya Kilimo ambapo kuna dawati mahsusi kwa ajili ya kuhamasisha kilimo hicho.

"Tunaipongeza Serikali tunaona ni jambo nzuri lakini pia kuna mkakati wa kitaifa ambao umekuwa ukionesha ni kwa namna gani Serikali imedhamiria kukipa kipaumbele kilimo hiki.

"Tunaipongeza Serikali ila tunaomba juhudi zaidi ziongezwe kwani tunatambua madhara ya kemikali zinazotumika katika masuala mbalimbali,"amesisitiza Liundi.

Akifafanua kuhusu Mradi wa Wanawake wa vijijini kuleta mabadiliko (RWCC), amesema TGNP inashirikiana na Shirika la Usimamizi Shirikishi wa matumizi ya Ardhi Tanzania (PELUM TZ) .

"Kupitia mradi huu TGNP tunafanya kazi kwa pamoja na PELUM TZ tukiangazia ni namna gani masuala Jinsia yanaweza kuingia katika kilimo ikolojia,"amesema Liundi.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa RWCC, Catherine Kasimbazi amesema lengo la mradi huo ni kuwafikia wakulima wanawake 5364.

Amesema mradi huo wa miaka sita ulianza Julai 2021 na unatekelezwa katika mikoa wa Kilimanjaro, Manyara pamoja na Morogoro .

"Tunatarajia kuwafikia wakulima wanawake Kwa wanaume 26,820 kupitia mradi huu wa kilimo ikolojia ,"amesema.










No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad