HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, May 12, 2024

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI IBADA YA KUWEKWA WAKFU ASKOFU MSAIDIZI JIMBO KUU KATOLIKI DODOMA

 

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Wazazi na Walezi nchini kuongeza jitihada katika malezi na makuzi bora ya watoto ili kukabiliana na changamoto ya ukatili unaowezeshwa na mitandao unaotishia usalama wa watoto ambapo watoto wanarubuniwa ili kujihusisha na vitendo viovu.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibada ya kuwekwa Wakfu Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Mhashamu Askofu Wilbroad Kibozi iliyofanyika Kituo Cha Hija Miyuji Mbwanga mkoani Dodoma. Amewasihi wazazi na walezi kutenga muda kujenga urafiki na watoto, ili kufahamu maendeleo yao, marafiki zao, na kuwawezesha kuwa huru kueleza changamoto zozote wanazopitia na hivyo kuweza kuwasaidia mapema. Amesema matumizi mabaya ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, na mwingiliano holela wa mila na desturi za mataifa mbalimbali zimeendelea kuathiri malezi na makuzi ya watoto pamoja na kudhoofika muunganiko wa kindugu au kirafiki kati ya wazazi na watoto wao ambao umepelekea watoto kukosa upendo na ulinzi wa wazazi au walezi.

Aidha Makamu wa Rais amehimiza vijana kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato halali kitakacho wawezesha kujikimu kimaisha. Amesema ni vema vijana wakajikita katika kazi za staha bila kuchagua zikiwemo za kilimo cha mbogamboga na matunda, na ufugaji wa wanyama aina mbalimbali za ndege na viumbe maji. Pia ametoa rai kwa watanzania kuzingatia muda wakati wa kuzalisha mali na utoaji huduma ili kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa Dini kuendelea kuhamasisha usafi, upandaji miti na utunzaji wa mazingira bila kuchoka na kuwaomba kukemea utupaji hovyo wa taka, uchomaji wa misitu na ukataji hovyo wa miti hususan kwa kutumi misumeno ya mnyororo ambayo imegeuka kuwa silaha mbaya ya kuangamiza misitu. Aidha amesisitiza suala la Taasisi zote za umma na za kidini (zikiwemo nyumba za Watawa, Seminari, Shule na Vyuo) ambazo zinalisha zaidi ya watu 100 kwa siku, kuhama kutoka matumizi ya nishati chafu, yaani mkaa na kuni, kwa ajili ya kupikia na kuanza kutumia nishati safi, yaani gesi asili, bio gas na umeme ili kufikia lengo la Taifa la 80% ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

Makamu wa Rais amesema Serikali inathamini mchango mkubwa wa Kanisa Katoliki, na madhehebu mengine ya Dini, katika utoaji wa huduma za kijamii na malezi bora. amesema Serikali itaendelea kusimamia na kulinda haki ya kuabudu kwa wananchi wote kwa mujibu wa Katiba na kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi katika mazingira ya haki na amani.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Kanisa na madhehebu mengine ya Dini ndiyo dhamiri ya jamii hivyo ni vyema Viongozi wa Dini kuishi wito wa kinabii kwa kusema na kuutetea ukweli kwa ajili ya maslahi ya wananchi hasa wanyonge. Aidha amewasihi kuendelea kuwakumbusha waamini na Watanzania kwa ujumla kwamba haki inaambatana na wajibu. Amewaomba viongozi dini kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani na utangamano, ikiwa ni pamoja na kuwaombea viongozi wa Serikali waweze kutekeleza vema majukumu ya kuwatumikia Watanzania kwa unyenyekevu na bila upendeleo.

Makamu wa Rais amempongeza na kumtakia heri Askofu Wilbroad Henry Kibozi kwa kuwekwa Wakfu na kukabidhiwa kazi ya Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dodoma ambapo amemuhakikishia Serikali itaendeleza ushirikiano wa dhati katika utekelezaji wa majukumu yake.

Ibada hiyo imehudhuriwa na Maaskofu na Mapadre kutoka maeneo mbalimbali nchini, Watawa, Viongozi wa Dini zingine, Viongozi wa Serikali, Waumini pamoja na wananchi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad