HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 9, 2024

Barrick yakabidhi msaada wa vifaa vya kisasa vya kupima ulevi wa madereva kwa Jeshi la Polisi

 

Meneja Mawasiliano (Corporate Communication and Country Liaison Manager) wa Barrick, Georgia Mutagahywa (wa pili kutoka kushoto) akimkabidhi moja ya vifaa vya kisasa vya kupima ulevi kwa madereva vilivyotolewa na Barrick kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani kanda maalum ya Dar es Salaam, Mohamed Bahashwan, katika hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa hivyo kwa Jeshi la Polisi iliyofanyika katika Kituo cha Oysterbay jijini Dar es Salaam , wengine pichani ni Kamanda wa Polisi wa Kinondoni SACP Mtatiro Kitinkwi (kushoto) na Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani wa Dar es Salaam SACP William Mkonda.

Na Mwandishi Wetu.

Katika kuendeleza mkakati wa kuhamasisha jamii kuzingatia usalama wakati wote, kampuni ya Barrick kupitia kampeni yake ya ‘Journey to Zero’ imekabidhi Jeshi la Polisi msaada wa vifaa vya kupima ulevi kwa madereva wa vyombo vya moto vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 katika hafla iliyofanyika katika kituo cha polisi cha Oysterbay kilichopo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akiongea katika hafla ya kupokea vifaa hivyo,Kamanda wa Polisi wa kanda ya Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mtatiro Kitinkwi,alisema msaada huyo wa vifaa vya kisasa vya kupima kilevi umetolewa kwa wakati mwafaka ambao Jeshi hilo linaendelea na mikakati ya kukomesha vitendo vya ulevi kwa madereva wanaoendesha vyombo vya moto ambao umekuwa ni chanzo kikubwa cha ajali nyingi za barabarani zinazotokea nchini.

“Tunawashukuru Barrick kwa kuendelea kuwa wadau wakuu wa kusaidia kampeni za ualama barabarani nchini na sisi tunawahodi kuwa vifaa hivi tutavitumia vizuri ili vifanikishe lengo lililokusudiwa la udhibiti wa madereva kutumia vinywaji vyenye kilevi kupita kiasi”.alisema Kitinkwi.

Alisema Jeshi la Polisi kupitia kikosi chake cha Ualama Barabarani pia litaendelea kutoa elimu ya unywaji kistaarabu kwa madereva wa vyombo vya moto ili kuhakikisha ajali nyingi zinazotokana na ulevi zinatokomezwa nchini na alitoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizi kwa kuwa suala la usalala linamgusa kila mwananchi.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano (Corporate Communications and Country Liaison Manager) wa Barrick, Georgia Mutagahywa, alisema kuwa msaada huo ni mwendelezo wa kampeni ya Barrick ya Journey to zero ambayo inalenga kuhamasisha afya na usalama kwa wafanyakazi wake na wadau wengine wote kwenye jamii.

“Kampeni yetu ya 'Journey to Zero' inalenga kuhakikisha wafanykazi wote wa kampuni wanakuwa salama wakati wote wanapokuwa kazini hadi wanaporudi nyumbani hivyo tumehakikisha kampeni hii inavuka mipaka hadi nje ya kampuni kuhakikisha jamii nzima inakuwa salama na ndio maana tunaendelea kuunga mkono Serikali kupitia Jeshi la Polisi kupambana na changamoto ya ajali za barabarani.

Mutagahywa alisema Barrick, siku zote itaendelea kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali kuunga mkono kampeni hizi za usalama barabarani na inaamini vifaa hivi vya kisasa vya kupima kilevi vilivyokabidhiwa kwa Jeshi la Polisi vitasaidia kuwabaini madereva wanaoendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa na kuchukuliwa hatua za kisheria ili kudhibiti na kupunguza matukio ya ajali za barabarani.

Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Kamati za Usalama barabarani nchini, Idd Azzan, aliishukuru Barrick, kwa kutoa msaada huo na kwa kuwa mdau mkuu wa kusaidia kampeni ya usalama , alitoa rai kwa watumiaji wa vifaa hivyo kuvitunza vizuri ili kuweza kufanikisha malengo mazuri yaliyokusudiwa sambamba na kuwarahisishia kazi, “Katika dunia ya sasa ya matumizi ya teknolojia nina imani vifaa hivi vitarahisisha kazi ya polisi wetu kuwanasa madereva walevi” alisisitiza.
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Kamati za Usalama barabarani nchini, Idd Azzan akiongea katika hafla hiyo.
Maofisa mbalimbali waandamizi wa Jeshi la Polisi wakifuatilia matukio katika hafla hiyo
Maofisa mbalimbali waandamizi wa Jeshi la Polisi walipata fursa ya kuongea katika hafla hiyo.
Viongozi wa kamati za usalama barabarani, Jeshi la Polisi na Barrick walipata fursa ya kupiga picha ya pamoja na wageni waliohudhuria katika hafla hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad