Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa ameeleza kuwa jumla ya mita za umeme 500 zimepokelewa kutoka kampuni ya CRJE (East Africa) L.T.D ambayo imepata kazi ya kusambaza mita hizo ambazo zinatarajiwa kwenda kufungwa katika mradi wa REA mkoani Geita.
Bi. Stella Kahwa amesema kuwa uhakiki wa mita mia tano (500) za umeme umefanyika kwa muda wa siku moja na mteja kukabidhiwa mita zake. Pia, ameeleza kuwa Wakala ina uwezo wa kupima mita nyingi za umeme kwa kutumia muda mfupi kwakuwa ina mitambo ya kisasa ambapo miwili ipo katika kituo cha uhakiki wa Vipimo Misugusugu na mmoja upo katika jengo la WMA Mkoani Kilimanjaro.
Katika mita 500 zilizowasilishwa asilimia 95 zimepita kwenye zoezi la uhakiki na zimewekewa rakili (seal) kwa ajili ya kuzilinda zisichezewe na asilimia 5 ya mita hazijaruhusiwa kuingia katika matumizi mpaka zitakapofanyiwa marekebisho na kuletwa tena kwa ajili ya zoezi la uhakiki na endapo zitakidhi vigezo zitaruhusiwa kutumika.
Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa wito kwa wadau wanaopata tenda za kusambaza mita za umeme kuhakikisha mita zao zinaletwa kwa ajili ya uhakiki ili kujiridhisha kama zinapima kwa usahihi kama Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 inavyoelekeza ili kuhakikisha mteja anapata vipimo sahihi katika mita na Shirika la Umeme (TANESCO) linakusanya fedha kulingana na matumizi sahihi ya umeme yanayotumiwa na wateja wao.






No comments:
Post a Comment