HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 28, 2024

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Imeahidi Kukabiliana na Hali ya Ugumu wa Maisha

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akijumuika na Familia ya Mzee Daudi Suleiman Ali, alipofika nyumbani kwake Fuoni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja kwa ajili ya kumsalimia na kumjulia hali yake leo 23-2-2024.(Picha na Ikulu) 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kukabiliana na hali ya ugumu wa maisha kwa kadri ya hali itakavyoruhusu, ili kuwapunguzia mzigo mzito wananchi wake.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu ya Pagali, Pemba alipozungumza na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi, CCM.

Rais Dk. Mwinyi amesema kupanda kwa gharama za maisha kunachangiwa na changamoto nyingi za uchumi duniani, zikiwemo, vita, kupanda bei kwa bidhaa za nje na baadhi ya mataifa duniani kuzuia kuuza bidhaa zao kwa mataifa mengine, akitolea mfano nchi ya India iliyozuia kuuza bidhaa zake kwa mataifa mengine duniani.


Alieleza, hali hiyo kuchangia kuzorotesha uchumi wa mataifa mengi na bei kupanda maradufu.


Aidha, alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafanya kila linalowezekana kustawisha uchumi na hali za wananchi kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo, Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuimarisha hali ya uchumi kwa wananchi.


Akizungumzia changamoto ya bandari ya Mkoani na hali ya kupanda kwa bei za bidhaa nchini, Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia wazee hao na wananchi wa kisiwa cha Pemba kwamba Serikali yao ina nia ya kuleta meli ya moja kwa moja kutoka bandari ya Mombasa hadi bandari ya Mkoani kwaajili ya kushusha bidhaa ili kuwapunguza gharama za maisha na mfumko wa bei za bidhaa hizo.


Pia, Rais Dk. Mwinyi aliwaomba wazee hao kuendelea kuiombea dua nchi ili amani iendelee.


Kwa upande wa wazee hao walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa hatua kubwa ya Maendeleo ya nchi ilivyopiga ndani ya muda mfupi.


Aidha, wazee hao walipongeza hatua ya Serikali kuendelea kuwalipa pensheni jamii, na kumshukuru, Rais Dk. Mwinyi kwa kuwaongezea kima cha pencheni hiyo.


Pia, wazee hao walitumia fursa hiyo kumpa pole Rais Dk. Mwinyi kwa msiba wa baba yake mzazi uliotokea hivi karibuni.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU, ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad