HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 15, 2024

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA TET KWA UTENDAJI KAZI WAKE

Kamati ya Kudumu ya Bunge  ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeipongeza Taasisi ya Elimu (TET) kwa utendaji kazi uliotukuka, hasa katika eneo la utekelezaji wa Mitaala iliyoboreshwa na uandaaji wa vitabu vya kiada kwa wanafunzi wa elimu ya Awali na Msingi.

Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 15, 2024 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Husna Sekiboko aliyeambatana na wajumbe wa kamati pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, Naibu Waziri wake, Makatibu Wakuu wa Wizara hiyo pamoja na wajumbe wa menejimenti ya TET walioongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Aneth Komba.

Akitoa pongezi hizo katika Ofisi za TET Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Husna Sekiboko amesema kuwa, kamati ya Bunge imeridhishwa na utendaji wa TET na kuwapongeza kwa kufanya kazi  kwa weledi katika kipindi  cha maboresho ya Mitaala yaliyofanyika miaka miwili iliyopita na utekelezaji wake ulioanza Januari 2024.

“Kwa kweli TET imefanya kazi nzuri sana  katika suala la uboreshaji elimu hapa nchini, hasa katika kipindi hiki ambacho tunahitaji wanafunzi waweze kujitegemea baada ya kupata elimu yao kutokana na kupata ujuzi.”Amesema Mhe. Sekiboko. 

Pia, ameitaka TET kuhakikisha inaweka lengo la ugawaji wa vitabu vya kiada kwa wanafunzi nchi nzima kufikia uwiano wa kitabu kwa mwananafunzi mmoja badala ya sasa kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Prof. Adolf Mkenda ameipongeza TET kwa utendaji wake mzuri na wa weledi, ikiwemo katika eneo la mafunzo kwa njia ya darasa la kidigitali (smart class) ambalo linaunganisha madarasa mia tatu kwa wakati mmoja.

“Madarasa hayo  ya kidigitali  yatasaidia sana katika kuhakikisha wanafunzi wote nchini wanajifunza kwa kupitia digitali na kurahisisha eneo la ufundishaji na ujifunzaji.” Amesema Prof. Mkenda.

Nae, Mwenyekiti wa Baraza la TET, Prof. Maulid Mwatawala ameishukuru kamati ya bunge kwa kuitembelea Taasisi hiyo, huku akiwahakikishia kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyoyatoa.

Awali akiwasilisha hali ya utendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dkt. Aneth Komba, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwaajili ya utekelezaji wa Mtaala ulioboreshwa ikiwemo  eneo la mafunzo na uchapaji wa vitabu vya kiada.












No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad