Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dk.Dotto Biteko amezitaka kampuni zinazojihusisha na uzalishaji wa mitungi ya gesi ya kupikia kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia nchini.
Akizungumza Mbagala jijini Dar es Salaam wakati akikagawa mitungi ya gesi ya Oryx 100 kwa Mama na Baba Lishe ambapo amesema kampeni ya nishati safi ya kupikia ni ya nchi nzima na safari yake ilianzishwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan baada ya kuzindua mpango wa nishati safi ya kupikia kwa wanawake wa Afrika akiwa katika mkutano wa kidunia.
“Mpango huu wa nishati safi Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan aliuzindua katika mkutano wa kidunia uliofanyika mwaka jana na mwaka huu atahudhuria tena mkutano wa 29 na Rais amekuwa akiifanya kampeni hii ya kuhamasisha nishati safi ya kupikia.”
“Madhara yanayotokana na nishati chafu mtu wa kwanza kuyapata ni mama.Wanawake wengi wanapata madhara ya kiafya kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi,”amesema Dk.Biteko na kuongeza wanawake wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta kuni na mkaa na kukutana na changamoto mbalimbali ikiweo ya kubakwa na wakati mwingine kushambuluwa na wanyama wakali.
“Niwashukuru Oryx kwa kuungana pamoja nasi kwa kutoa mitungi ya gesi kwa mama lishe kwani hiki ni kiashiria kuwa safari ya nishati safi Tanzania imeanza na imeanzia hapa Mbagala, itakwenda na mahali kwingine kwa ajili ya kuwapatia nishati safi wanawake wa Tanzania.”
Aidha amewaomba viongozi wa Serikali pamoja na taasisi kuelewa kwamba ajenda ya nishati safi sio ya Serikali peke yake bali ni ajenda ya wote, hivyo waisukume kuhakikisha mwanamke wa Tanzania anapata hadhi.
“Ni matumaini mitungi hii ya gesi ambayo tumeigawa leo itakuwa ni chachu ya kuchochea nishati safi ya kupikia.Hivyo niendelee kuziomba kampuni nyingine zinazozalisha mitungi ya gesi ama nishati nyingine yasibaki nyuma.Wafanye kila wanaloweza kuhakikisha wanawake wa Tanzania wanapata nishati safi na wanapata maendeleo.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Oryx Gas Benoite Araman amesema kupika kwa gesi ya Oryx ni kulinda mazingira kwa kuacha kukata miti huku akisisitiza zaidi ya yote ni kulinda afya ya wanawake kwa kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao unaotokana na kuni na mkaa.
“Wanawake wanatumia muda mchache kupika hivyo wanapata nafasi kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kuepuka kugombana na wenza wao kwa kuchelewesha chakula, na wanaume pia watajiongezea marks ukiwazadia wamama mitungi ya gesi.Kwa kutumia gesi ya Oryx, Watoto wanakua na muda mwingi zaidi kusoma na sio kwenda kutafuta kuni,”amesema Benoit.
“Kuanzia Julai mwaka 2021 tumekuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya Serikali tulioyapokea toka kwa Raisi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuwa ifikapo mwaka 2023 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Kupitia mipango hii, Oryx Gas inataka kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa ambayo si tu mbaya kwa afya zetu bali pia ni hatari kwa mazingira yetu na pia Oryx Gas inatekeleza juhudi za kueneza matumizi ya nishati safi kwa Watanzania wengi ipasavyo ambayo ni ndoto kubwa ya Mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan.”
No comments:
Post a Comment