HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 23, 2024

VIJIJI VYOTE 360 IRINGA VYAPATA UMEME

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akikata utepe kuashiria uwashaji umeme katika Kijiji cha Mkangwe wilayani Mufindi mkoani Iringa tarehe 22 Februari 2024.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mkangwe wilayani Mufindi mkoani Iringa baada ya kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho, kukagua miundombinu ya umeme pamoja na kufungua zahanati ya Kijiji husika tarehe 22 Februari 2024.

*Zaidi ya asilimia 64 ya vitongoji vyote vina umeme
*Dkt. Biteko ataka kasi ya usambazaji iendane na mahitaji
*Atuma Salamu uchaguzi Serikali za Mitaa

USAMBAZAJI umeme vijijini mkoani Iringa umefanyika kwa asilimia 100
ambapo vijiji vyote 360 mkoani humo vimesambaziwa umeme kupitia miradi
mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Usambazaji umeme katika vitongoji vya Mkoa huo umetekelezwa kwa
asilimia 64.11 ambapo vitongoji 1,188 vimesambaziwa umeme kati ya
1,853.

Hayo yametanabaishwa wakati wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko mkoani Iringa kwa ajili
kuwasha umeme na kukagua miundombinu ya umeme.

Baada ya kuwasha umeme kwenye Kijiji cha Mkangwe wilayani Mufindi,
Dkt. Biteko amewataka wakandarasi wa miradi ya usambazaji umeme
vijijini kutekeleza kazi kwa wakati ili kuendana na kasi ya maendeleo
huku akiiagiza REA kuwachukulia hatua wakandarasi wazembe.

Aidha, amewapongeza Wakandarasi wa umeme vijijini waliofanya kazi ya
usambazaji mkoani Iringa ambayo imepelekea vijiji vyote mkoani humo
kuwa na umeme kufikia Desemba 2023.

Akiwa katika Kijiji cha Mkangwe, Dkt. Biteko alizindua Zahanati ya
Kijiji cha Mkangwe ambapo aliagiza uongozi wa Halmashauri wilayani
Mufindi kuhakikisha Zahanati hiyo inaanza kuhudumia wananchi ipasavyo
kufikia jumatatu ya tarehe 26 Februari 2024 baada ya huduma ya umeme
kufika kwenye zahanati hiyo na hii ikijumuisha kuwepo kwa Rasilimali
Watu na Vitu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa Wanachama wa Vyama
mbalimbali vya Siasa kwenye mkoa huo kupendana na kushirikiana katika
shughuli za kiuchumi na kijamii na kamwe itikadi zao za vyama
zisiwafanye watengane na kutoshirikiana.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Dkt.
Biteko amewaasa wananchi kuchagua viongozi wanaowasikiliza,
wanaotambua changamoto zao na jinsi ya kuzitatua; pia amewataka
wagombea kutozungumza lugha za maudhi wakati wa uchaguzi huo kwani
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka maridhiano kwenye nchi na si
kugawanyika.

Hafla ya uwashaji umeme katika Kijiji cha Mkangwe wilayani Mufindi
ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Halima Dendego, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Mbunge wa
Mufindi Kusini, Mhe.David Kihenzile na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad