HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, February 18, 2024

PROF.MDOE AFUNGA MAFUNZO YA UONGOZI, USIMAMIZI YALIYOTOLEWA KWA WALIMU 369

 









Na Mwamvua Mwinyi
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe, amefungua mafunzo ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Shule yanayoendeshwa na ADEM kwa Walimu Wakuu wa Mkoa wa Tanga katika Chuo cha Ualimu Korogwe.

Amepongeza hatua ya Walimu Wakuu hao kupatiwa mafunzo ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa shule kwani Uongozi na Usimamizi bora wa elimu ni chachu ya kufikia mafanikio ya elimumsingi nchini.

Prof. Mdoe amesema Menejimenti ya ADEM imefanya jambo jema kwa kuandaa na kuendesha mafunzo hayo kwa Walimu Wakuu nchini na kuwataka washiriki kwenda kuyaweka kwenye vitendo ili kuleta tija ya mafunzo hayo na hivyo kufikia adhma ya Serikali ya kuendeshwa kwa mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yanaendeshwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ikihusisha Walimu Wakuu 369 kutoka Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Muheza Vijijini, Muheza Mji na Kilindi kuanzia tarehe 15-17 Februari, 2024.

Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Siston Masanja Mgullah akizungumza wakati wa hafla hiyo ya ufunguzi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha Walimu Wakuu kusimamia vyema na kwa ufanisi shule zao na ametumia fursa hiyo kuwaasa Walimu Wakuu wanaoshiriki mafunzo hayo kuhakikisha hadi wanapohitimu mafunzo hayo wawe wamepata maarifa ya kutosha, uzoefu wa namna ya kuendesha na kusimamia shule zao na ujuzi kuhusu Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Shule wanazosimamia kupitia mada mbalimbali zinazofundishwa na wawezeshaji wa mafunzo pia kwa kubadilishana uzoefu na walimu wakuu wenzao.

Dkt. Masanja ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawajengea umahiri walimu wakuu katika maeneo ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa shule, Uandaaji wa Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Shule, Motisha kwa Walimu, Usimamizi wa Rasilimali za Shule, Usimamizi wa Ufundishaji na Ujifunzaji, Usimamizi wa miradi ya ujenzi, kusimamia ustawi wa Wanafunzi shuleni na Ushirikishwaji wa jamii katika kuleta maendeleo ya shule.

Mwenyekiti wa washiriki wa mafunzo Bw. Richard Mlangwa ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule Msingi Zavuza iliyopo Wilayani Handeni ameshukuru kwa walimu wakuu kupewa mafunzo kwani yatawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hivyo kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Mafunzo hayo yataendeshwa pia katika Mikoa ya Kigoma, Mtwara, Simiyu, Kilimanjaro na Mbeya na yatahusisha jumla ya Walimu Wakuu 4,620 kutoka katika Mikoa hiyo kupitia mradi wa BOOST.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad