HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 27, 2024

HISTORIA YAANDIKWA; JNHPP YAINGIZA MEGAWATI 235 GRIDI YA TAIFA

 *Serikali yatekeleza ahadi kabla ya siku tatu

*Megawati 235 nyingine kuingizwa Machi, 2024
*Uzinduzi rasmi kufanyika mwezi Machi mwaka huu
*Dkt. Biteko asema hakuna kulala; vyanzo vipya kutekelezwa
*Mkandarasi apongeza usimamizi wa Dkt.Biteko

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema
kuwa, mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa megawati
2,115 umeanza kazi na kuingiza megawati 235 katika gridi ya Taifa
kupitia mtambo Namba 9.

Hatua hii ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kuwa mtambo huo ungeanza
kuzalisha umeme tarehe 25 Februari 2024, ahadi iliyotimizwa siku tatu
kabla kuanzia tarehe 22 Februari 2024 mtambo huo ulipoanza
uzalishaji.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 25 Februari 2024 wakati akitoa taarifa
ya utekelezaji wa mradi huo kwa baadhi ya wakuu wa vyombo vya Habari
na Wahariri katika eneo la mradi wilayani Rufiji mkoani Pwani ambapo
wahariri hao walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo
Bwawa la kuhifadhi maji yatakayozalisha umeme, Tuta Kuu na mitambo ya
umeme.

Ameeleza kuwa, kuingia kwa megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa
kumeboresha hali ya upatikanaji umeme nchini na kupunguza upungufu wa
umeme kwa zaidi ya asilimia 85.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere unaendelea na
ifikapo mwezi Machi 2024 megawati nyingine 235 zitaingia katika gridi
kupitia mtambo namba 8 na kufanya JNHPP kuingiza megawati 470 kwenye
gridi na hivyo kupelekea nchi kuwa na ziada ya umeme ya megawati 70.

Amesema utekelezaji wa mradi huo ni jitihada za Rais, Dkt.Samia Suluhu
Hassan ambaye alikuta mradi huo ukiwa na aslimia 33 na sasa mradi huo
unafikia mwisho.

Amesema, Dkt. Samia anaijali nchi kwa dhati na sasa mipango yake ya
maendeleo haiangalii kipindi cha sasa tu bali miaka 30 hadi 40 ijayo
na ndio maana ameshaagiza uendelezaji wa vyanzo vipya vya umeme
ikiwemo Gesi, Maji na Nishati Jadidifu inayojumuisha Jua, Upepo na
Jotoardhi.

Dkt. Biteko pia amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini
ya Hayati, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wa kutekeleza mradi huo
ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2018.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameeleza kuwa, utekelezaji wa JNHPP
hauifanyi Wizara ya Nishati na Taasisi zake kubweteka na kutegemea
umeme kutoka mradi huo pekee bali kasi ya utekelezaji wa miradi
mingine mipya inaendelea ikiwemo mradi wa Rumakali (222MW), Ruhudji
(358) na miradi ya Jotoardhi ya Ngozi na Kiejo-Mbaka pamoja na mradi
wa umeme Jua wa Kishapu (150MW).

Kuhusu utunzaji wa mazingira, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Wahariri wa
Vyombo vya Habari kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa
mazingira ambao ndio unasababisha mabwawa ya umeme kuwa na maji ya
kutosheleza kuzalisha umeme na pia kutoa elimu kuhusu athari za
kuharibu vyanzo vya maji vinavyopeleka maji pia katika mabwawa ya
umeme.

Kwa wananchi wanaozunguka maeneo yenye mitambo ya kuzalisha umeme,
Dkt. Biteko amesisitizaTANESCO ihakikishe hawapati changamoto ya umeme
kwani hao ndio walinzi wa maeneo hayo na mradi unapofika katika eneo
lolote lazima ubadilishe hali ya wananchi katika eneo husika kwa namna
mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa huduma za kijamii.

Dkt. Biteko ameipongeza TANESCO na kampuni ya usimamizi wa mradi ya
TECU kwa utekelezaji na usimamizi madhubuti wa mradi ambao umewezesha
kuingiza megawati 235 kwenye gridi.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema kuwa, ujazo
wa maji unaohitajika katika Bwawa la umeme la JNHPP ni mita za ujazo
bilioni 32.7 na sasa kuna mita za ujazo bilioni 28 hivyo bado mita nne
tu Bwawa hilo kujaa kabisa.

Amesema kuwa, makadirio ni kuwa mita nne zilizobaki zitajaa mwezi huu
kupitia usimamizi madhubuti wa Bonde la Maji la Rufiji.

Ametoa wito kwa wananchi kutunza vyanzo vya maji na kutofanya
uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji pia wasichepushe maji
kiholela.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa,
mradi huo ni muhimu katika kutekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan ya kuifanya Pwani kuwa Mkoa wa kimkakati kwa kujenga
viwanda vingi zaidi ambavyo kufanya kwake kazi kunategemea nishati ya
umeme ya uhakika.

Amesema kuwa, mahitaji ya umeme mkoani Pwani ni megawati 130 lakini
bado hayatoshelezi mahitaji hivyo mradi wa JNHPP kupitia kituo cha
umeme cha Chalinze kitawezesha Mkoa huo kupata umeme wa uhakika ambao
utachochea wawekezaji wapya.

Ameongeza kuwa, kwa sasa Mkoa wa Pwani una viwanda 1,533 ambapo
katika Serikali ya Awamu ya Sita viwanda 30 vinajengwa huku 17 vikiwa
ukingoni kumalizika hivyo mradi wa JNHPP ni muhimu katika kufanya
viwanda hivyo kufanya uzalishaji.

Meneja Mradi kutoka kampuni zinazotekeleza mradi huo (Arab Contractors
na Elsewedy Electric) Mohamed Zaky, amesema kuwa kampuni hiyo inaona
fahari kufikia hatua hiyo ya uzalishaji na kwamba nia yao ni kutimiza
ndoto ya Tanzania kuzalisha megawati 2115 kupitia mradi wa JNHPP.

Aidha, amempongeza Dkt. Doto Biteko kwa msukumo anaoutoa kwa
wakandarasi hao ili kutekeleza mradi kwa wakati na pia kwa kuusimamia
kwa karibu mradi husika.

Viongozi wengine walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu
Mteule Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, Kamishna wa Umeme na
Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mwenyekiti wa Bodi ya
TANESCO, Dkt. Rhimo Nyansaho na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,
Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
akitazama ujazo wa maji katika bwawa kwenye mradi wa Julius Nyerere
ambao umeanza kuingiza megawati 235 kwenye gridi ya Taifa.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
akitangaza kuhusu mradi wa Julius Nyerere kuingiza megawati 235 kwenye
gridi ya Taifa katika eneo la mradi, Rufiji mkoani Pwani.
Muonekano wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad