HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 30, 2024

LST YASHIRIKI KUBORESHA MFUMO WA HAKI JINAI NCHINI

 
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), Prof. Sist Mramba ametembelea maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma kuanzia Januari 24-30 mwaka huu. Maonesho hayo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya sheria illiyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania na yanatarajiwa kuhitimishwa ifikapo siku ya sheria nchini Februari Mosi, 2024.

Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) imeendelea kushiriki katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai nchini kupitia mafunzo yanayowawezesha wanafunzi wanaofaulu mitihani yao kuwa na sifa za kuajiriwa na kufanya kazi za sheria katika utumishi wa umma au kuwa Mawakili wa kujitegemea ambao pamoja na mambo mengine hushughulikia mashauri mbalimbali yakiwemo yanayogusa haki jinai.

Akizungumza katika maonesho ya Wiki ya Sheria nchini yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma, Kaimu Mkuu wa Taasisi ya LST, Prof. Sist Mramba alisema kuwa taasisi hiyo ni mdau mkubwa wa Mahakama na imeshiriki maadhimisho hayo ili kutoa elimu na ushauri wa masuala mbalimbali ya kisheria kwa wananchi.

“Kufikia Desemba 2023 jumla ya wanafunzi wa LST wapatao 8,717 walifaulu mafunzo yao na kutunukiwa Stashahada ya Uzamili ya Sheria kwa Vitendo (Post-Graduate Diploma in Legal Practice). Tuzo hiyo inawawezesha kuwa na sifa za kufanya kazi za sheria katika utumishi wa umma au kuwa Mawakili wa kujitegemea,” alibainisha Prof. Mramba.

Pia alisisitiza kuwa LST ina imani kubwa juu ya mchango unaotolewa na Mawakili pamoja na Wanasheria wa Serikali katika kupambana na vitendo vya uvunjifu wa haki za wananchi na kuhakikisha haki hizo zinatetewa, zinalindwa na zinapatikana kwa wakati kupitia mkondo wa sheria kwa kushirikiana na Mahakama.

Aidha, Prof. Mramba alifafanua kuwa kupitia kituo cha msaada wa kisheria cha Taasisi hiyo (LST Legal Aid Centre) wananchi mbalimbali wenye uhitaji wameweza kunufaika na huduma ya msaada wa kisheria wakiwemo wahanga wa masuala ya haki jinai hususan wanawake na watoto.

Kwa upande wao wananchi waliotembelea maonesho hayo wameipongeza Mahakama kwa kuandaa maonesho na taasisi zote zilizoshiriki kutoa elimu ya sheria kwa Watanzania, pia wamefurahia huduma na ushauri waliopata kutoka kwa washiriki hao.

Maonesho hayo yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kufanyika kuanzia tarehe 24 hadi 30 Januari mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini kwa lengo la kuziweka pamoja taasisi zote ambazo ni wadau wa sheria na haki ili ziweze kubadilishana uzoefu, kuona njia bora ya utendaji kazi kwa pamoja na kuwawezesha wananchi kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Tanzania: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai” na yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi mnamo tarehe 1 Februari, 2024 ambayo ni siku ya sheria nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad