HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 12, 2024

DC MTATIRO AWAONYA WAZAZI WASIOPELEKA WATOTO WAO SHULE

 

Baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ligoma wilayani humo.


Na Mwandishi wetu, Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro,ametoa wiki moja kwa wazazi wilayani humo kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza,kuanza masomo ya elimu ya awali na msingi wanakwenda kuripoti kwenye shule walizopangiwa kabla hawajachukulia hatua za kisheria.

Mtatiro ametoa kauli hiyo jana,akiwa katika ziara ya kukagua mahudhurio ya watoto wa elimu y awali,darasa la kwanza na wale waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza katika shule mbalimbali wilayani humo.

Mtatiro alisema,jumla ya wanafunzi 4,834 wanatakiwa kujiunga na shule za sekondari za kutwa wilayani humo,kati yao wavulana 2,379 na wasichana ni 2,455.

Mtatiro alisema,serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, imejenga jumla ya madarasa mapya 16 kwa ajili ya wanafunzi hao katika shule mpya mbili za sekondari katika kata ya Tinginya na Tuwemacho.

Kwa mujibu wa Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wlaya hiyo alisema,madarasa mengine 134 yatakayotumika ni yale yaliyokuwa yanatumiwa na wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2023 ambayo yameandaliwa kwa ajili hiyo.

Katika hatua nyingine Mtatiro ametaja watoto wanaotakiwa kuanza elimu ya awali ni 11,356 ambapo wavulana ni 5,708 na wasichana ni 5,646 na kwa darasa la kwanza ni 10,815,wavulana 5,398 na wasichana 5,417.

Ameipongeza Halmashauri ya wilaya ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Chiza Marando,kwa kazi nzuri iliymaofanya katika ujenzi wa miundombinu bora ya elimu ambayo inatoa nafasi kwa walimu kuwa na mazingira bora ya kufundishia na watoto kupata nafasi ya kujifunzia.

Mkuu wa wilaya,amewaonya wazazi na walezi,kuacha visingizio kwa sababu walishafahamu kwamba mtoto/watoto wao wanapaswa kwenda shule mara baada ya matokeo ya mitihani ya darasa la saba na walitakiwa kufanya maandalizi mapema.

“wazazi ni lazima wahakikishe kila mtoto anapelekwa shule kupata elimu ambayo ni haki yake ya msingi badala ya kubaki nyumbani,serikali haitamvulimia mzazi mzembe atakayeshindwa kupeleka mtoto wake kuanza elimu ya awali,msingi na sekondari”alisema Mtatiro.

Amewaagiza watendaji wa vijiji,kata na maafisa tarafa kuwafuatilia watoto wote wenye sifa ya kuanza elimu ya awali,msingi na sekondari wanakwenda shule ili kupata haki zao za masingi.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza Marando alisema,madarasa na matunndu ya vyoo katika shule zote za msingi na sekondari ujenzi wake umekamilika na yako tayari kwa matumizi.

Marando,amemshukuru Rais Dkt Samia kwa kuipatia Halmashauri hiyo fedha za kutosha zilizowezesha kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu ambapo amewataka wazazi kutumia fursa hiyo kupeleka watoto wao shule.

Alisema,serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha imejenga miundombinu na kuajiri walimu wa kutosha,hivyo ni jukumu na wajibu wa wazazi na walezi wanashiriki katika kuinua suala zima za elimu katika wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad