Na Karama Kenyunko Michuzi tv.
WAFANYABIASHARA watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka nane likiwemo la kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya Sh bilioni 1.167.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali Mwandamizi, Medalakini Emmanuel akisaidiana na Jeniva Rugalama na Auni chilamula imewataja washtakiwa hao kuwa ni Emmanuel Nkalang’ano, Rugainunula Lwekamwa na Mwita Nyakiha.
Washtakiwa wanakabiliwa na makosa ya kuhujumu uchumi ikiwemo kuongoza genge la uhalifu, kutoa risiti za uongo, kutumia kifaa cha kielektroniki kwa njia ya kupotosha mfumo, kuisababishia mamlaka husika hasara na utakatishaji fedha.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Joyce Mushi inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2022 na Agosti 2023 huko Kariakoo Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja walipanga njama za uhalifu kwa kutoa risiti za uongo kwa nia ya kujipatia faida.
Inadaiwa, katika kipindi hicho washtakiwa kwa pamoja walitoa risiti za uongo kutoka kampuni ya Vartual Fiscal Device iliyosajiliwa kwa jina la Rugainunula kwa nia ya kumdanganya Kamishna kuwalipa walipakodi wengine Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Sh 150,987,915.31/-
Pia, inadaiwa washtakiwa, Nkalang’ano, Rugainunula na Nyakiha kwa pamoja walitoa risiti za uongo za Vartual Fiscal Device kwa kampuni iliyosajiliwa kwa jina la Rugainunula kwa nia ya kumlaghai Kamishna ili kuwalipa walipa kodi wengine Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) 1,167,537,867.58/-
Katika shtaka la kutumia vifaa vya kielektroniki, washyakiwa kwa njia ya kupotosha mfumo, inadaiwa walitumia Vartual Fiscal Device iliyosajiiwa kwa jina la Rugainunula kutoa risiti za uongo za fedha zilizopakiwa katika mfumo wa TRA ili kuwaongezea walipa kodi ili kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Tsh 150,987,915.31/-
Pia inadaiwa kati ya Januari 2023 na Agosti 2023 katika eneo hilo hilo, washitakiwa wote walitumia Vartual Fiscal Device iliyosajiliwa kwa jina la Rugainunula kutoa risiti za uongo zilizopakiwa katika mfumo wa TRA hivyo kusababisha walipa kodi wengine kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Sh bilioni 1.16/-
Katika mashtaka ya kuisababishia hasara mamlaka inadaiwa kuwa, katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2022 na Desemba 2022 kwa makusudi washtakiwa waliisababishia TRA hasara ya Sh 150,987,915.31/-.
Pia, inadaiwa kuwa kwa kitendo hicho, waliisababishia TRA hasara ya Sh bilioni 1.167.
Aidha, washitakiwa wote wanadaiwa kuafanya muamala wa fedha kiasi cha Sh 150,987,915.31 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu.
Inadaiwa washtakiwa wote kwa pamoja pia, wanadaiwa kujihusisha na muamala wa Sh bilioni 1.167 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa.
Hata hivyo Hakimu washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwamba haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa sababu mashitaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
No comments:
Post a Comment