HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, December 10, 2023

TPF Net CHALINZE YAWAASA WANAFUNZI KUJIEPUSHA NA MAKUNDI HATARISHI

 Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
MTANDAO wa Polisi wanawake (TPF Net) Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mkoani Pwani, umetoa rai kwa wanafunzi wa kujiepusha na makundi hatarishi ambayo yanaweza kuwa chanzo cha kukatisha masomo yao ama kushuka kitaaluma.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sophia Lyidenge alitoa rai hiyo ,wakati akikabidhi viti 20 katika shule ya Sekondari Chalinze, kata ya Bwilingu kwa wanafunzi wa shule hiyo, ikiwa ni maadhimisho ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Vilevile aliwaasa ,wanafunzi kujiepusha na makundi hatarishi yanayoweza kupelekea kukatisha masomo yao ama kushuka kitaaluma.

Lyidenge aliwataka pia kusoma kwa bidii ambapo aliwakumbusha wanafunzi hao kukitumia vyema kipindi cha likizo wakiwa majumbani ,kujikumbusha masomo waliyofundishwa badala ya kuwa wakaidi na kujiingiza kwenye vitendo viovu vya utumiaji wa mihadarati, wizi pamoja ngono.

Alikemea vitendo vya unyanyasaji watoto, kuwatumisha watoto wakiwa wadogo kwa kuwaachisha masomo yao.

Lyidenge alitoa rai kwa jamii kujenga tabia ya kufichua vitendo vya kikatili vinavyofanywa kwa watoto , kwani mtoto wa mwenzio ni wako.

"Tuwafichue wale wote wenye vitendo vya unyanyasaji kwenye jamii, hii itasaidia kuwachukulia hatua za kisheria na kukomesha tatizo hili "alisisitiza.

Nae Mkuu wa shule ya Sekondari Chalinze, Sudi Said alilishukuru Jeshi la Polisi Wilaya ya Chalinze kwa namna walivyoguswa kusaidia wanafunzi hao.

Akizungumza wakati wa kupokea viti hivyo, Diwani wa Kata ya Bwilingu, Nassa ameupongeza mtandao huo na kueleza tukio kama hilo kwa siku za nyuma ilikuwa siyo rahisi kuona likifanywa na Jeshi la Polisi bali na asasi zingine za serikali na za kiraia.

Alisema Jeshi la Polisi limempa somo kubwa kwa jambo walilolifanya na watakua ni mfano wa kuigwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad