HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 8, 2023

MAAFISA VIUNGO WA WAHIMIZWA KUKUTANA NA KAMATI ZA MALIASILI NA MAZINGIRA ZA VIJIJI KUJENGA UELEWA MRADI WA SLR


Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili na Mazingira kutoka Kijiji cha Nkungusi Kata ya Sibwega, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi, Bw. Saleh Mbuya akichangua mada wakati wa mafunzo kwa kamati za maliasili na mazingira za vijiji zinazotekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka Bonde la Ziwa Rukwa. Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Ijumaa Desemba 8, 2023 Jijini Mbeya.

Na Mwandishi Wetu, Mbeya
MAAFISA Viungo wa Halmashauri zinazotekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wametakiwa kuitisha mikutano ya mara kwa mara na Kamati za Maliasili na Mazingira za Vijiji ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Desemba 8, 2023 na Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda wakati akifungua mafunzo kwa Kamati za Maliasili na Mazingira kutoka Vijiji 20 vilivyopo katika Bonde la Ziwa Rukwa zinazotekeleza mradi huo ikijumuisha Halmashauri za Wilaya ya Sumbawanga (Rukwa), Tanganyika (Katavi) na Mpimbwe (Katavi).

Dkt. Mapunda amesema ni wajibu wa Maafisa viungo kuhakikisha kamati za maliasili na mazingira za vijiji zinapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wa Serikali za vijiji ili kuhakikisha kuwa elimu ya uhifadhi wa mazingira na urejeshaji wa uoto wa asili inawafikia wananchi wanufaika kupitia mradi huo.

“Nawahimiza Maafisa viungo kutambua umuhimu wa kufanya mikutano na kamati za maliasili na mazingira za vijiji pamoja na serikali za vijiji ili kuhakikisha kunakuwepo na uelewa wa kutosha kuhusu mradi huu ambao una manufaa makubwa kijamii na kiuchumi” amesema Dkt. Mapunda.

Aidha Dkt. Mapunda amewataka maafisa viungo kuhakikisha viongozi wa kamati za maliasili na mazingira za vijiji wanatambua vyema jukumu lao katika usimamizi na utekelezaji wa mradi ili kuwawezesha wananchi kuendesha shughuli zao za kijamii na kiuchumi kupitia uvuvi, kilimo, ufugaji na kupata mazao yenye tija.

Kwa mujibu wa Dkt. Mapunda amesema mradi huo ulianzishwa mahsusi na serikali ikiwa ni juhudi za za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu zisizo rafiki na mazingira ikiwemo ukataji miti, uchomaji mkaa na uharibifu wa vyanzo vya maji ambavyo vimekuwa tishio kwa uhai wa binadamu na viumbe hai.

Mradi pia umekusudia kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ambapo tutawezesha uboreshaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo pamoja na malisho ya mifugo ili kuzuia muingiliano wa shughuli za kijamii na kiuchumi kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo vyanzo vya maji” amesema Dkt. Mapunda.

Kwa upande wake Mshauri wa Kiufundi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Doyi Mazenzele amesema Shirika hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuweka mikakati ya pamoja kwa kuendelea kuhimiza jamii kutambua umuhimu wa utunzaji wa bioanuai ambazo zinachangia upatikanaji wa huduma ikolojia ikiwemo maji, chakula, ustawi wa maisha bora na kipato kutokana na shughuli za kiuchumi.

“Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali kubwa ya maliasili za misitu, nyika, ardhi oevu, maziwa, mito na bahari ambavyo ni msingi wa utajiri wa maliasili…Tumekutana na kamati hizi ili kuwajengea uelewa wa pamoja ili kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa bioanuai katika mfumo wa misitu unaotokana na uvunaji haramu wa rasilimali ikiwemo kuni na mkaa” amesema Mazenzele.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Maliasili na Mazingira kutoka Kijiji cha Iziwasunku, Kata ya Kasansa Halmashauri ya Mpimbwe, Mkoani Katavi Bi. Metrida Juwakali ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais na IUCN kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuunga mkono juhudi za serikali katika uhifadhi wa mazingira na urejeshaji wa uoto wa asili.

Tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza jamii zetu umuhimu wa kukabiliana na uharibifu wa mazingira….Tukiwa kama viongozi tunapaswa kuwaelimisha wananchi tulionao kwani umuhimu na faida za utunzaji wa mazingira faida na manufaa yake ni yetu sote” amesema Bi. Juwakali.

Mradi wa SLR unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo kiasi cha Bilioni 25.8 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huo wa miaka mitano ulioanza mwaka 2021 unatarajia kukamilika mwaka 2025 ambapo jumla ya Mikoa 5, Halmashauri 7, Kata 18 na vijiji 54 vinatarajia kunufaika na mradi huo. Halmashauri zinazonufaika na mradi ni Iringa Vijijini (Iringa), Wilaya ya Mbeya na Mbarali (Mbeya), Halmashauri za Sumbawanga vijijini (Rukwa) pamoja na Halmashauri za Wilaya za Tanganyika na Mpimbwe (Katavi).
Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili na Mazingira kutoka Kijiji cha Mkusi Kata ya Kapemta, Halmashauri ya Sumbawanga Mkoani Rukwa, Bw. Edgar Christopher akichangua mada wakati wa mafunzo kwa kamati za maliasili na mazingira za vijiji zinazotekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka Bonde la Ziwa Rukwa. Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Ijumaa Desemba 8, 2023 Jijini Mbeya.
Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Damas Mapunda akizungumza jambo wakati wa mafunzo kwa kamati za maliasili na mazingira za vijiji zinazotekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka Bonde la Ziwa Rukwa. Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Ijumaa Desemba 8, 2023 Jijini Mbeya.
Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Damas Mapunda akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo kwa kamati za maliasili na mazingira za vijiji zinazotekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka Bonde la Ziwa Rukwa. Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Ijumaa Desemba 8, 2023 Jijini Mbeya. Kulia ni Mshauri wa Kiufundi kutoka Shirika la IUCN, Bw. Doyi Mazenzele na Dkt. Amuri Nyambila Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kilichopo Mkoani Morogoro.
Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Damas Mapunda akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Viungo na Wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) muda mfupi baada ya kufungua mafunzo kwa kamati za maliasili na mazingira za vijiji zinazotekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka Bonde la Ziwa Rukwa. Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Ijumaa Desemba 8, 2023 Jijini Mbeya. Kulia ni Mshauri wa Kiufundi kutoka Shirika la IUCN, Bw. Doyi Mazenzele na Dkt. Amuri Nyambila Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kilichopo Mkoani Morogoro.
(PICHA NA MPIGAPICHA WETU)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad