HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 22, 2023

WINS AUCTION MART KUKUSANYA DENI LA BIL. 7.8 KWA WADAIWA SUGU NYUMBA ZA TBA

 

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani,) kuhusiana na hatua za uhimizaji ulipaji wa kodi za pango kwa wakati kwa ustawi wa Wakala hiyo na Taifa kwa ujumla. Leo jijini Dar es Salaam.

DENI La shilingi Bilioni 7.8 lililotokana na malimbikizo ya madeni ya kodi za pango kwa nyumba na majengo ya Serikali limepekelea wasimamizi wa nyumba hizo ambao ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) kumtumia dalali wa Mahakama kukusanya fedha hizo Nchi nzima kwa mujibu wa sheria ili zitekeleze miradi mingine kwa manufaa ya watanzania kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro amesema, ulimbikizwaji wa madeni hayo kumekuwa kikwazo cha kutekeleza mipango ya maendeleo ikiwemo kujenga nyumba mpya kwa ajili ya kupangisha au kuuzwa pamoja na kukarabati nyumba zilizopo.

"Hadi kufikia Oktoba 31 mwaka huu TBA inadai zaidi ya Bilioni 7.8 za kodi ya pango kutoka kwa wapangaji wa nyumba na majengo yanayomilikiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) nchi nzima ambapo zaidi ya Bilioni 3.5 ni madeni ya Taasisi mbalimbali za Serikali." Amesema.

Kuhusiana na hatua ya kuwaondoa wadaiwa sugu kwa kutumia dalali wa Mahakama ambaye amepewa zabuni hiyo kwa niaba ya TBA; Arch Kondoro amesema kampuni ya udalali wa Mahakama ya WINS Auction Mart imeshakabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa kuanzia Desemba Mosi mwaka huu na hatua itakayofuata mara baada kuondolewa katika nyumba hizo kuwafungulia kesi za madai mahakamani wadaiwa hao ili kuhakikisha wanalipa madeni hayo.

"Madeni haya ni ya mwaka wa Fedha uliopita...Na Mikoa kinara ni taasisi za Umma katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya ambayo deni limefikia shilingi Bilioni 1.4......Nitoe rai kwa wapangaji wote zikiwemo taasisi za Umma kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati mara baada ya kupokea namba za kumbukumbu za malipo yaani control number ambazo hutumwa kwa kila mpangaji Kila mwezi kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS.)" Amefafanua.

Aidha, Arch. Kondoro ameeleza kuwa; Kuanzia Desemba 1, 2023, Wakala hiyo itaanza kutumia mfumo mpya wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Miliki za Serikali (GRMS) toleo la 2.

"Mfumo huu mpya utakuwa unatoza riba ya 20% kwa mpangaji atakae kaa zaidi ya miezi 3 bila kulipa kodi ya pango. Riba hiyo itaendelea kutozwa kila mwezi kwa kiwango mfuato (automatically) cha 20% mpaka deni lote litakapokamilika kulipwa. Utekelezaji huu ni kwa mujibu wa kifungu Na. 5.2 cha mkataba wetu wa upangishaji." Amesema.

Takribani nyumba 1716 zinazomilikiwa na TBA zimepangishwa kwa watumishi na viongozi wa Umma nchi nzima huku utekelezaji wa miradi hiyo ukiendelea nchi nzima na katika jitihada za kuepukana na ulimbikizwaji wa madeni ya pango TBA imekuja na ubunifu kwa miradi inayotekelezwa sasa kutumia vitasa janja (smartlock) kwenye majengo mapya ili kudhibiti malimbikizo ya kodi ya pango huku mpango huo wa kufunga vitasa janja ukidhamiriwa kutekelezwa katika nyumba za zamani

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad