HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 22, 2023

WAANDISHI HABARI ZA MTANDAONI WATAKIWA KUJIUNGA NA TOMA

 * Maadili, kanuni na teknolojia vyatajwa kufikia mafanikio


WAANDISHI wa habari za mtandaoni nchini wametakiwa kujiunga kupitia mwavuli wa taasisi ya Tanzania Online Media Alliance (TOMA,) ambao ni mtandao wa waandishi wa habari za mtandaoni ili kujijenga kitaaluma, na kuwa na sekta moja ya waandishi wa habari za mtandaoni yenye sauti moja ya kutetea maslahi yao.

Akizungumza wakati akifungua mpango mkakati huo Mkurugenzi wa Klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC,) Kenneth Simbaya amesema kuwa katika kuyafikia malengo ni muhimu waandishi wa habari kufanya kazi kwa manufaa ya Umma pamoja na kuzingatia sheria na kanuni hususani katika wakati huu ambao Sayansi na Teknolojia inakua kwa kasi.

Amesema, Uzinduzi wa mpango mkakati huo wa mtandao wa waandishi wa habari za mtandaoni umelenga kuwaunganisha wanahabari hao pamoja na kuwajengea uwezo wa kuandika habari zinazoendana na wakati na kuzingatia ubora wa matumizi kwa Umma wa watanzania.

"Sayansi na Teknolojia inakua kwa kasi, lazima tuzingatie nidhamu katika kufikisha ujumbe kwa jamii pamoja na kuzingatia weledi na sheria za habari...nazipongeza klabu za waandishi wa habari za mikoa yote kwa jitihada mnazochukua katika kuimarisha zaidi tasnia hii ya habari hususani klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha ambako imetoka taasisi hii ya TOMA." Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Freedom House ambao ni wadhamini wa mradi huo Daniel Lema amesema kuwa, lengo na kuzindua mpango mkakati huo ni kutoa mwelekeo wa namna ya utekelezaji wa shughuli za taasisi ya TOMA kwa miaka mitano ijayo.

"Mtandao huu kwa waandishi wa habari za mtandaoni umelenga kuwaunganisha wanahabari hao na kuwa na sauti moja na kutetea maslahi yao kote nchini kama sekta moja ya waandishi wa habari za mtandaoni." Amesema.

Aidha ameeleza kuwa TOMA imelenga kuboresha habari zinazotolewa na waandishi wa habari za mtandaoni kwa kuhakikisha zinahusisha sauti za pembezoni ambazo hazisikiki katika uga huo ikijumuisha makundi mbalimbali ikiwemo asasi za kiraia na watu waliopo pembezoni ambako sauti zao hazisikiki na kuhakikisha zinaletwa katika uga wa habari za mtandaoni.

Pia ametoa mwito kwa waandishi wa habari za mtandaoni kujiunga na chombo hicho ambacho kimeundwa kwa ajili yao na kuwataka wajiunge kwa manufaa ya kujijenga kitaaluma, kutoa na kujibu changamoto zinazowakabili.

Mmoja ya wanachama wa TOMA na Mkurugenzi wa Kijukuu Blog kutoka Kahama William Bundala amesema, uzinduzi huo wa mpango mkakati wa miaka mitano ijayo ni fursa kwa wanahabari za mtandaoni kwa kuwa inawaleta pamoja na kubadilishana uzoefu.

"Waandishi wa habari habari za mtandaoni tupo wengi, na kupitia TOMA tunaamini wanahabari wengi zaidi watajiunga katika idadi ya wanachama 260 tuliyopo ili kujenga zaidi tasnia hii ya habari za mtandaoni kwa kuzingatia sheria na kanuni za habari." Amesema.

Mkurugenzi wa Klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC,) Kenneth Simbaya akizungumza wakati akizindua mpango mkakati wa taasisi ya Tanzania Online Media Alliance (TOMA,) na kuwataka waandishi wa habari za mtandaoni kuzingatia weledi, kanuni na maadili katika kuwasilisha taarifa kwa jamii. Leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi mkaazi wa taasisi ya Freedom House Daniel Lema akizungumza wakati uzinduzi wa mpango mkakati huo na kueleza kuwa TOMA imelenga kuwaunganisha waandishi wa habari za mtandaoni na kuwa na sauti moja ya kutetea maslahi yao nchini kama sekta moja ya waandishi wa habari za mtandaoni. Leo jijini Dar es Salaam.

Mwanachama wa TOMA na Mkurugenzi wa Kijukuu Blog William Bundala akizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa mpango mkakati huo na kutoa mwito kwa waandishi wa habari kujiunga na mtandao huo ili kujijenga zaidi kitaaluma na kubadilishana uzoefu. Leo jijini Dar es Salaam.

Matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati wa taasisi ya Tanzania Online Media Alliance (TOMA.) Leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad