HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 13, 2023

MUHAS KUSHEREHEKEA MIAKA 60 TANGIA KUANZISHWA KWAKE

  

Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Apolinary Kamuhabwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati wa kutoa taarifa juu ya kusheherekea miaka 60 ya kuanzishwa kwake.


Na Karama Kenyunko Michuzi tv
CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimesema kinaposherehekea miaka 60 ya kuanzishwa kwake, kinajivunia maendeleo mbalimbali ya sekta ya afya ikiwemo kuzalisha madaktari bingwa na bobezi na wataalamu wa afya ngazi zote.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam, Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema chuo hicho ni kikongwe nchini na kwamba walianza na wanafunzi 10 wa diploma ya utabibu lakini mpaka sasa wanadahili wanafunzi 4,000 kila mwaka.

"Kwa miaka hii tumetoa wataalamu mbalimbali wa afya, tulianza na programu moja na sasa tunazo programu 101 na kati ya hizo 81 ni za uzamili na uzamivu hivyo, tumetoa wataalamu katika hospitali za rufaa, wizarani na madaktari bobezi," amesema Profesa Kamuhabwa.

Ameeleza pia, baada ya chuo hicho kuanzishwa kumekuwa na ongezeko la vyuo vya afya baada ya wao kutoa rasilimali watu hivyo imechangia maendeleo ya sekta ya afya.

Aidha, akielezea matukio yatakayoambatana na sherehe za miaka 60, Profesa Kamuhabwa amesema watakuwa matukio mawili ya Novemba 16 na 18, mwaka huu ili kufanya tathmini kuhusu mafanikio waliyopata tangu walivyoanza.

Ameeleza kuwa watakuwa na kongamano litakalohusisha wadau mbalimbali wakiwemo wahitimu wa zamani, wa kati na wakaribuni, wadau walioshirikiana nao, taasisi za serikali na binafsi, wadau wa maendeleo, wanafunzi na wazazi.

Amesema lengo la kongamano hilo ni kutafakari mafanikio waliyopata na changamoto walizopitia na namna walivyozitatua.

Pia amesema kuwa wataangazia kwenye programu za mafunzo, idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kwa upande wa miradi ya tafiti, wahitimu wanaotoka wanaenda wapi na wanafanya nini.

"Mdahalo utafanyika Novemba 16, 2023 ambao utalenga maeneo hayo na kikubwa ni kuangalia tulipotoka, tulipo na tunapoelekea kwa miaka ijayo, taasisi iwe ya namna gani," amesisitiza.

Profesa Kamuhabwa amesema baada ya mdahalo huo watakuwa na mkutano wa mwaka kwa wahitimu waliomaliza chuo hicho ili kutoa fursa ya namna ya kukifikisha chuo mahali wanapotaka.

Sambamba na hilo, watakuwa na maonesho mbalimbali yatakayooneshwa na skuli na taasisi kuhusu bidhaa wanazozalisha na bunifu zinazofanyika.

Amesema chuo hicho kina wataalamu wabobezi, vifaa tiba vya kupima maradhi mbalimbali hivyo, watatoa huduma za kupima watu kuangalia afya zao bure kwa magonjwa yasiyoambukiza.

Aidha, amesema Novemba 18, 2023 watakuwa na matembezi ya hisani kama kumbukizi ya miaka 60 ambayo yatafanyika kwa Kilometa 1, 5,10 na 15 katika viwanja vya chuo hicho.

Ameeleza kuwa wanatarajia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo na wageni zaidi ya 500.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad